Habari

Kahawa yageuka chungu kwa wakuzaji

March 6th, 2018 2 min read

Na MWANGI MUIRURI na IRENE MUGO

WAKULIMA wa kahawa katika eneo la Mlima Kenya sasa wameamua kuacha kilimo hicho kinachowapa hasara na kuwafanya maskini.

Zaidi ya viwanda 10 vimefungwa katika maeneo mengi ya Mlima Kenya kutokana na kuongezeka kwa madeni, usimamizi mbaya, bei duni ya zao la kahawa na uchuuzi wa zao hilo.

Katika eneo la Mathira, chama cha akiba na mikopo cha Mathira North Coffee Farmer’s Co-operative Society kiko katika hatua za mwisho kuporomoka.

Viwanda vyake vitatu vimeshafungwa baada ya asilimia 99 ya wakulima kujiondoa wakilalamikia malipo duni.

Mambo ni mabaya zaidi katika kaunti ya Murang’a, ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wakulima wameng’oa zao hilo kutoka ekari 750.

Wanaripotiwa kutupilia mbali kilimo hicho ili kukumbatia uwekezaji katika sekta ya ujenzi wa nyumba na pia kujiingiza katika kilimo cha mimea mingine yenye faida.

Hatua hii ni hatari kubwa kwa jitihada za Kaunti hiyo kufufua kilimo cha kahawa hadi kurejelea kilele chake cha miaka ya 1980 ambapo Kaunti hiyo ilikuwa ikizalisha asilimia 80 ya mavuno ya kahawa yote hapa nchini.

Miaka hiyo, Murang’a ilikuwa ikivuna tani 200 za kahawa na pato lake lilikuwa la kupendeza kiasi kwamba mashirika ya wakulima wa kahawa yalikuwa yakikopesha serikali pesa.

Ripoti hiyo ya afisa wa ustawishaji kilimo cha kahawa katika Kaunti, Paul Mutua akitoa ukadiriaji wa sekta hiyo katika kufunga mwaka wa kifedha wa 2016 -17, alisema kuwa bei duni, ushindani wa nafasi za ujenzi na kilimo cha mboga na matunda na pia kukosekana kwa imani ya wakulima kunahatarisha kilimo cha kahawa katika eneo zima la Mlima Kenya.

Anasema kuwa hali ikiendelea katika mtindo huo ambapo katika mwaka wa 2015 ekari 350 zilikuwa zimeng’olewa miti ya kahawa, basi kabla ya
2030 kufika, kilimo hicho kitakuwa kimefifia.

Ripoti hiyo inaangazia hatari hiyo kuwa, kabla ya mwaka 2022, kutoka idadi ya sasa ya wakulima 70,000 wanaolima kahawa, watakuwa wamepunguka hadi chini ya 40,000.

Ingawa bei ya kahawa sokoni imekuywa ilkiripotiwa kupanda kwa kasi, ile bei ambayo humfikia mkulima imesemwa kuathiri sana bidiii za wakulima kuzalisha zao hili.

Ripoti hiyo inasema kuwa licha ya kilo moja ya kahawa lkatika mnada kubakia zaidi ya Sh120, katika Kaunti ya Murang’a mkulima amekuwa akifikiwa na Sh50 mwaka wa 2012 kwa kilo moja, ikapunguka hadi Sh30 mwaka wa 2013 na kisha ikapanda tena hadi Sh42 mwaka wa 2014.

Mwaka wa 2015 bei hiyo ilipanda tena hadi Sh55, ikashuka tena hadi Sh45 mwaka wa 2016 lakini kwa sasa bei ni Sh30.