Michezo

Kahawa yalenga kumaliza ligi bila kushindwa

August 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KOCHA wa Kahawa Queens, Joseph Wambua Mwanza amesema kikosi chake kimepania kuendeleza mtindo wa kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wao kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu huu.

Kocha huyo amedokeza katika mpango mzima wanataka kukamilisha kampeni za muhula bila kushindwa.

Kahawa Queens ambayo tayari imefuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu muhula ujao imebakisha mechi tatu kumaliza ratiba ya kipute hicho ambapo amedai anaamini wachezaji wake watatimiza azma yao.

”Bila kujipigia debe kama kocha ninawahimiza wachezaji wangu wajiweka vizuri kukabili upinzani wowote utakaokuja mbele yao kwenye mechi zilizosalia,” kocha huyo alisema na kuongeza kwamba kamwe hawezi kudharau wapinzani wao maana nao pia wamejipanga kutafuta ushindi ili kujiongezea tumaini la kumaliza katika nafasi bora muhula huu.

Kahawa imepangwa kucheza na Joy Love, Mukuru Talent na Moving the GoalPost (MTG) United.

Kwenye mkumbo wa kwanza, Kahawa chini nahodha, Dorcas Awuor ilichapa Joy Love magoli 5-0 kisha kubeba magoli 4-0 na 2-0 dhidi ya MTG na Mukuru Talent mtawalia.

Kahawa Queens ilithibitishwa kuibuka malkia wa kipute hicho majuma majuma yaliyopita ilipokanganya Limuru Starlets kwa magoli 7-0 na kufikisha jumla ya alama 33 baada ya kucheza mechi 11.

Kahawa Queens imewafungua kabisa wapinani wa karibu, MTG yenye alama 22 ambapo hata ikishinda mechi zake tatu itafika pointi 31.