Michezo

Kahawa yazidi kupiga wapinzani

September 2nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanawake ya Kahawa Queens ilijiongezea matumaini ya kumaliza mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza bila kushindwa iliyotwaa ufanisi wa bao 1-0 dhidi ya Mukuru Talent Academy uwanjani Kahawa Barracks, Nairobi.

Kahawa Queens ya kocha, Joseph Wambua Mwanza ambayo tayari imetwaa ubingwa wa kipute hicho na kunasa tikiti ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu msimu ujao ilitolewa kijasho na wapinzani wao ambao hutiwa makali na kocha, Amos Abongo.

Wachezaji wa pande walishuka dimbani tayari kutafuta ufanisi wa pointi tatu muhimu huku wakiteremsha mashambulizi ya kufa mtu. Vigoli wa Mukuru Talent Academy wanaokamata nafasi ya tano kwa alama 17 walionekana karibu kulemea wenyeji wao ndani ya kipindi cha pili lakini wapi kila wakati walishindwa kupenya difensi ya Kahawa Queens.

Kunako dakika ya 58, Kahawa Queens chini ya nahodha, Dorcas Awour kilifanya kweli pale Lucy Mukhwana alipojaza kimiani bao la ushindi baada ya kupata krosi safi kutoka kwake Joan Naututu.

“Kusema kweli napongeza wachezaji wangu kwa kazi njema waliofanya licha ya kuonekana kuzidiwa nguvu na wapinzani wetu hatimaye walifanikiwa kujipatia alama zote na kutimiza azma yetu,” alisema kocha wa Kahawa.

Kahawa Queens ambayo imebakisha patashika moja dhidi ya Moving The Goalposts (MTG) United ingali kifua mbele bila kupoteza alama yoyote ambapo imekusanya pointi 39 baada ya kucheza mechi 13.