Habari za Kitaifa

Kaimu Inspekta Jenerali awataka polisi kuzingatia sheria wakiwa kazini


KAIMU Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli amewaagiza maafisa wa polisi kufuata sheria wakitekeleza majukumu yao, siku moja tu kabla ya  maandamano yanayopangwa ya Nane Nane.

“Kila Mkenya kwa mujibu wa sheria ana uhuru wa kuandamana, kulalamika na kukusanyika kulingana na sheria. Hilo kila mtu analifahamu sana. Na pale uhuru wa mmoja unapoishia, ndipo wa  mwingine unapoanzia. Tunatawaliwa na Mkataba wa Roma na Katiba ya Kenya,” akasema.

Bw Masengeli alizungumza wakati wa mkutano na makamanda wa  Polisi wa Kenya, Polisi tawala na Idara ya Upelelezi wa Jinai katika Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Polisi, Embakasi Jumanne, Agosti 6, 2024.

Mkutano huo ulifanyika kabla ya maandamano ya Nane Nane yanayotarajiwa kufanyika Alhamisi, Agosti 8, 2024.

Maandamano hayo yatakuwa mtihani kwa makamanda wa polisi huku huduma hiyo  ikilaumiwa vikali kwa jinsi ilivyoshughulikia maandamano ya hapo awali.

Bw Masengeli aliwaambia maafisa wa polisi wanaoendesha shughuli zao wakivalia kama raia kujitambulisha kila mara huku akibainisha kuwa huduma ya polisi ina nia ya kushughulikia masuala ya usalama nchini na kuhakikisha usalama wa Wakenya.

Kuhusu Gen Z, alisema,  ujumbe wao umesikika na ni jukumu la polisi kutofautisha kati ya Gen Z na wanaotumia maandamano kusababisha fujo, uharibifu wa mali na vurugu ambazo haziruhusiwi kisheria.

Alisema watakaotumia maandamano kushiriki uhalifu  watashughulikiwa kwa uthabiti na kutoa wito kwa umma kushirikiana na polisi kudumisha usalama  wa nchi.

Pia aliwahimiza polisi kukumbatia ubunifu katika kukabiliana na uhalifu unaojitokeza kama vile uhalifu wa mtandaoni, ugaidi, itikadi kali za kikatili na ujangili.

Alisisitiza kujitolea kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kushirikiana na idara nyingine ndani ya mfumo wa Haki ili kuwahudumia Wakenya vyema na kutaja Idara ya Mahakama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na magereza kama washirika wakuu.

Mkutano huo ulioangazia,  “Hali ya Usalama wa Kitaifa-Changamoto, Fursa na Mikakati” ulikusudiwa kupitia baadhi ya changamoto kubwa za usalama zinazoikabili nchi na zinazohitaji uangalizi wa haraka miongoni mwao kuongezeka kwa machafuko ya kiraia, uhalifu wa mtandaoni na vitendo vya kigaidi.

Wakati huo huo, Katibu wa Masuala ya Kigeni, Dkt Korir Sing’oei ameitaka Serikali kudhibiti mikusanyiko na maandamano nchini,  akisema inasababisha changamoto za kiuchumi.

Katika taarifa  kwenye akaunti yake ya X, katibu  huyo, alisema maandamano hayo yameathiri uchumi, hasa katika sekta ya kibinafsi.

“Moja ya sababu za kudhibiti na kukabiliana na maandamano na machafuko ni kwamba waandamanaji hawazingatii gharama za vitendo vyao,” alisema.

“Gharama hizi zinabebwa na watu wengine – sekta ya kibinafsi. Kama vile uchafuzi wa mazingira, maandamano yenye vurugu yanahitaji kudhibitiwa kabla ya kusababisha gharama zisizoweza kurekebishika.