Michezo

Kakamega Homeboyz yanusurika nao Wazito wakivuna

March 2nd, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

KAKAMEGA Homeboyz ilitoka nyuma Jumapili na kuzamisha Nzoia Sugar 3-2 ugani Bukhungu kwenye mechi ya Ligi Kuu (KPL), na kuzidisha presha kwa viongozi wa ligi, Gor Mahia.

Katika mechi nyingine zilizosakatwa kwenye viwanja mbalimbali, wenye ngwenje Wazito waliwazidi maarifa Zoo Kericho 4-1 katika mechi ya kwanza ugani Kenyatta, Machakos kisha Bandari wakatitiga KCB 2-1 ugani humo.

Mathare United nayo ilitoka sare ya 1-1 na Posta Rangers uwanjani Ole Ntimama mjini Narok.

Kwenye mechi ya Homeboyz, mshambulizi Benjamin Oketch, Allan Wanga na Kennedy Onyango walifunga mabao matatu kipindi cha pili na kuwaokoa vijana hao wa Nicholas Muyoti baada ya Peter Gin na Philip Muchuma kuweka Nzoia Sugar kifua mbele kipindi cha kwanza.

Bandari chini ya mkufunz Twahir Muhiddin nayo ilipata ushindi wake wa tatu mfululizo kutokana na mabao mawili ya Johanna Mwita kipindi cha pili. Samuel Odhiambo aliwafungia KCB bao la kufutia machozi kabla ya Bandari kukomboa na kupata la ushindi.

Matokeo hayo yalikuwa mabaya kwa KCB ambao ushindi ungewapaisha hadi mbele ya Ulinzi Stars na Tusker na kuwaweka pazuri katika kutoa upinzani kwa Gor Mahia na Kakamega Homeboyz.

Hata hivyo, ni Wazito waliojivunia ushindi mkubwa dhidi ya Zoo Kericho ambao sasa wanakodolewa macho na hatari ya kushushwa ngazi wakiendelea kupata matokeo mabaya.

Vijana wa kocha Stewart Hall walipata mabao yao manne kupitia Denis Ng’ang’a, mshambulizi matata Mungai Kiongera, Austin Out na nguvu mpya Joe Waithira kujihakikishia ushindi huo mnono. Bao la kufutia machozi la Zoo lilimiminwa wavuni na Collins Neto.

Hata hivyo, kipa wa Zoo Kericho Vincent Misikhu alifanya masihara mengi langoni na mashabiki wamezua maswali kuhusu namna alivyokubali kufungwa mabao rahisi huku madai ya upangaji matokeo ya mechi yakizidi kushamiri kwenye KPL.

Huu ulikuwa ushindi wa pili kwenye mechi sita uliosajiliwa na Wazito ambao wamesuasua sana msimu huu na walionekana kuamka baada ya kuadhibu Chemelil Sugar 6-0 mnamo Februari.

Wazito bado wanashikilia nafasi ya 13, pengo la alama 10 likitamalaki kati yao na Zoo ambao wako kwenye hatari ya kushushwa ngazi.

 

Mathare United 1 Posta Rangers 1

Wazito 4 Zoo Kericho 1

Kakamega Homeboyz 3 Nzoia Sugar 2

KCB 1 Bandari 2