Michezo

Kakamega Homeboyz yawapiga wenyeji Mathare United

November 29th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KAKAMEGA Homeboyz imeandikisha ushindi wake wa kwanza kabisa ikicheza dhidi ya Mathare United ugenini kwenye Ligi Kuu baada ya kuchapa mabingwa hao mwaka 2008 kwa mabao 3-1 uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Ijumaa.

Homeboyz, ambayo illingia Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2013 ilikuwa imejaribu kupiga Mathare ugenini mara tano, lakini bila mafanikio.

Peter Thiong’o alipatia Homeboyz bao la kwanza sekunde chache kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika kupitia kichwa kisafi alipopokea krosi kutoka kwa Stephen Etyang’.

Thiong’o aliimarisha uongozi wa Homeboyz dakika ya 52 kabla ya Mathare kufufua matumaini kupitia kichwa cha John Mwangi aliyepokea krosi kutoka kwa Marvin Ongori dakika ya 62. Mwangi alikuwa amejaza nafasi ya Clifford Alwanga dakika ya 57.

Wenyeji Mathare walipata pigo zikisalia dakika 10 pale Roy Okal alionyeshwa kadi yake ya pili kwenye mechi hiyo kwa kucheza visivyo.

Dakika mbili baadaye, David Okoth alizamisha kabisa Mathare alipopachika bao la tatu.

Ushindi huu ni wa pili mfululizo wa Homeboyz dhidi ya Mathare baada ya kuchapa klabu hiyo kutoka kaunti ya Nairobi 2-1 uwanjani Bukhungu mwezi Machi.

Homeboyz sasa imerejea katika nafasi ya pili kwenye ligi hii ya klabu 17 kutoka nambari sita baada ya ushindi huu. Imezoa alama 20 kutokana na mechi 11. Iko nyuma ya mabingwa watetezi Gor Mahia wanaongoza kwa alama 24 kutokana na mechi tisa.

Mathare, ambayo iliingia mchuano huo ikishikilia nafasi ya nne, imerushwa hadi nambari saba. Inasalia na alama 17.

 

Ratiba ya Jumamosi, Novemba 30

Wazito na Chemelil Sugar (3.00pm, Machakos)

Kariobangi Sharks na KCB (3.00pm, Kasarani)

Nzoia Sugar na AFC Leopards (3.00pm, Mumias Sports Complex)

Gor Mahia na Ulinzi Stars (3.00pm, Kisumu)