Dondoo

Kakangu huenda kwa mganga akitaka kuniangamiza, polo aambia kijiji

June 13th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

NYATIKE, MIGORI

Kalameni mmoja kutoka hapa aliwashangaza wazee alipowaambia kwamba ndugu yake huenda kwa mganga akitaka kumwangamiza amrithi mkewe.

Kulingana na mdokezi, polo aliitisha kikao na wazee ili kujadili mienendo ya ndugu yake. Polo alidai kwamba mtu fulani aliyejitambulisha kama mganga maarufu alimpigia simu na kumtahadharisha dhidi ya kula pamoja na ndugu yake.

“Sijui mganga huyo alipata wapi nambari yangu. Lakini aliniambia kwamba ndugu yangu humtembelea akitaka nipatwe na ugonjwa mbaya ili nilemazwe,” polo alidai.

Polo, alidai kwamba ndugu yake hufanya haya yote ili apate wakati mzuri wa kumrithi mke wake. Vicheko vilisikika kikaoni huku wazee wakimtaka polo afafanue zaidi kuhusiana na madai aliyoibua.

“Hata nyinyi nimeona mmeungana na huyu mtu. Kama ni hivyo acha mkutano huu ukamilike na nimshughulikie jinsi nijuavyo,” polo aliwafokea wazee.

Inasemekana ndugu yake alisimama na kuwaeleza wazee kwamba polo alikuwaa amepagawa. “Huyu jamaa ninashuku ameingiwa na mashetani. Kama sio hivyo, basi ameanza kuvuta bangi,” ndugu ya polo alidai.

Lakini jamaa alidai kwamba si simu ya mganga pekee ambayo ilimfanya kushuku ndugu yake. Alisema mara kwa mara amekuwa akipokea simu kutoka kwa majirani wakimueleza jinsi polo alivyopenda kuingia kwa boma lake.

“Nikiwa kazini huwa ninapata hadithi nyingi sana. Yeye hufanya nini na mke wangu?” polo alichemka.

Inadaiwa wazee walimshauri polo afanye uchunguzi wa kina bila kumhusisha mtu yeyote. “Hakuna uchunguzi nitafanya,” polo alipandwa na mori na kumzaba kaka kofi. Wazee wote walilazimika kutorokea usalama wao.

…WAZO BONZO…