Dondoo

Kalameni ajuta kuwatongoza binti za mama pima

July 17th, 2018 1 min read

Na DENNIS SINYO

Matungu, Mumias

Jombi aliyefika kwa mama pima kupata dozi, alitimuliwa kwa kumtongoza binti wa mama huyo.

Inasemekana kwamba mama pima alikuwa na wasichana warembo sana ambao hakutaka mtu yeyote kuongea nao bila idhini yake. Hata hivyo, jamaa huyo aliamua kujaribu bahati mama alipokuwa akihudumia wateja wengine.

Kulingana na mdokezi, jamaa alianza kurushia mwanadada mmoja mistari mfululizo ili amwingize box. Licha ya kuonywa kwamba alikuwa akicheza na moto, jamaa alijitia hamnazo.

Inasemekana mama pima alimpata akiongea na binti yake na akakasirika. Alimwamrisha msichana kuondoka kisha akaanza kumfokea jamaa. “Wewe ulikuja kunywa pombe au kusumbua wasichana wangu? Kama hujui kilichokuleta hapa, nitakuonyesha,’’ alifoka mama huyo.

Jamaa akidhani ni mzaha, mama alichukua pombe yake na kuimwaga chini na kumwamuru aondoke mara moja. “Usicheze na mimi. Ninaweza kukupa adabu ambayo hutasahau maishani mwako. Nakwambia simama na utoke

hapa mara moja!” mama huyo aliamuru.

Jamaa alikataa mara ya kwanza lakini mama akawa mkali zaidi. Alimnyanyua juu kwa shati na kumsukuma nje. Alimuonya kwamba akirejea wake angekiona cha mtema kuni.

Kioja hicho kilimfanya jamaa kusalimu amri na kuondoka kwa uchungu huku akirushiwa maneno mazito mazito. “Usidhubutu kurejea hapa. Unakuja hapa na Sh50 na unajifanya kuwa sonko kumbe huna kitu ila kusumbua watoto wangu tu,” mama alimweleza.

Mama huyo ana wasichana watano warembo anaowachunga sana huku yeyote anayedhubutu kuwasumbua akijipata pabaya

Kulingana na mdokezi, jamaa huyo aliponea kwani mama huwacharaza wanaume wanaowatamani mabinti zake wakiwa kwake. “Kwanza wewe una bahati sana.

Huyo mama angekucharaza kwa nyahunyo watu wakiangalia,” jamaa huyo aliambiwa na makalameni wenzake baada ya kuondoka kwa mama pima.