Dondoo

Kalameni aliyetamani dadake akemewa

June 15th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MAKADARA, ATHI RIVER

JOMBI wa hapa alikemewa na marafiki wake kwa kudai kwamba alikuwa akivutiwa kimapenzi na dada yake.

Jamaa alikuwa akipiga gumzo na wenzake mjadala ulipozuka kuhusu vipusa waliokuwa wakiwavutia mtaani.Kila mmoja alitaja kipusa aliyekuwa akimtamani na kupatiwa mawaidha na wenzake jinsi ya kumnasa.

Jamaa alichangamka na kusema alikuwa hakukuwa na mwanadada wa kumvutia mtaani isipokuwa dada yake.

“Marafiki wake waliposikia kauli ya jamaa walifikiri alikuwa akifanya mzaha lakini akashikilia kwamba hakukuwa na kidosho mrembo kama dada yake mtaani,” alisema mdokezi.

Marafiki wake walipogundua jamaa hakuwa akifanya mzaha, walimkemea vikali wakimweleza anafaa kuheshimu dada yake.

Walimweleza kwamba alikuwa na mawazo mabaya sana kwa kufikiria kuwa na uhusiano wa kimapenzi na dada yake. “ Hapa hatumzungumzii upendo wa mtu na ndugu au dada yake, tunazungumzia uhusiano wa kimapenzi unaoweza kufanya watu wawili kuoana na kuishi kama mume na mke. Wewe unasema unampenda dada yako, haujui kwamba ni makosa mtu kuoa au kuhusika kimapenzi na dada yake na anaweza kushtakiwa kortini,” mmoja wa marafiki wake alimweleza jamaa.

Hata hivyo, jamaa alisema hata kama hawezi kumuoa dada yake, hakukuwa na msichana mrembo na mwenye umbo la kuvutia kama yeye mtaani. “ Ninataka mkubaliane name kwamba katika mtaa huu hakuna mwanamume asiyegeuza shingo kumtazama dada yangu akikutana naye njiani. Hata nyinyi hapa mnamtamani na hamkumtaja kwa sababu niko hapa,” jamaa alieleza.

Kulingana na mdokezi, makalameni walikubaliana na jamaa kwamba dada yake alikuwa mrembo na kwamba hakuna aliyekuwa amemrushia ndoano kwa sababu walikuwa wakimuogopa. Hata hivyo, walimweleza kwamba hafai kufikiria kumchumbia dada yake.