Dondoo

Kalameni atwangwa kama nyoka kufumaniwa na kisura wa sponsa

April 1st, 2018 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Zimmerman, Nairobi

POLO mmoja mtaani hapa, anauguza majeraha baada ya kulishwa kichapo kikali kwa kufumaniwa kwa kidosho anayelipiwa kodi ya nyumba na sponsa.

Inasemekana jombi ni mkubwa wa mwanadada huyo kazini. “Jamaa alikuwa akinyemelea kipusa huyo akitaka kuonja asali,” alieleza mdokezi wetu.

Kwa kuwa kimwana pia alimpenda kalameni huyo, alimkubali ingawa hakufichua alikuwa amewekwa na sponsa.

Yasemekana jamaa alikuwa akimtembelea kipusa mchana wakati wawili hao hawakuwa kazini. Licha ya kuonywa na majirani wa mwanadada huyo kuepuka nyumba hiyo jamaa alipuuza.

Siku ya kioja, kipusa alimshawishi jamaa amtembelee jioni ili akeshe kwake wakipiga moyo pasi kwa mapenzi. “Hawakujua sponsa alikuwa na wadaku wake plotini,” alisema mdokezi.

Inasemekana mwendo wa saa sita za usiku mapenzi yalipokuwa yameshika kasi, buda alifika baada ya kupakuliwa uhondo na wadaku wake.

Juhudi zake kubisha mlango afunguliwe na kidosho hazikufua dafu kwa sababu ya mahaba na sauti ya kinanda iliyotawala chumba cha kulala.

Sponsa hakuwa na budi ila kuagiza vijana alioandamana nao wavunje mlango. “Nyinyi mjipe raha tu, lakini mtajua mimi ndiye hulipa kodi ya hii nyumba,” alifoka buda vijana wake waking’ang’ana kufungua mlango.

Hatimaye mlango ulivunjwa na sponsa huyo akapata wawili hao wakijiburudisha.

“Umesema ukame ng’ombe usiyejua gharama ya kutunza?” alichemka buda akiangushia polo mangumi na mateke, huku akisaidiwa na vijana wake.

Purukushani hizo ziliamsha majirani waliomnusuru kalameni aliyekuwa hoi sakafuni.

Yasemekana jamaa huyo ambaye ana mke na watoto anaendelea kupokea matibabu katika hospitali moja humu jijini.

…WAZO BONZO…