Dondoo

Kalameni mjeuri akunja mkia

November 6th, 2019 1 min read

NA NICHOLAS CHERUIYOT

SOSIT, KERICHO

Kalameni wa hapa, alimchemkia mke wa rafiki yake akimlaumu kwa kutaka kumtenganisha na mwenzake.

Inasemekana jamaa na mume wa mwanadada wamekuwa marafiki tangu utotoni na wamekuwa wakisaidiana kukabiliana na pandashuka za maisha. “Urafiki wao umekuwa wa kupigiwa mfano na wengi eneo hili kwani huwa wanahusiana kwa ukaribu sana kama ndugu,” akaeleza mdokezi.

Miezi miwili iliyopita, rafiki ya kalameni alipata jiko alipojaliwa kumpata kidosho aliyeumbika ajabu.

Mrembo huyo hakufurahishwa na ukaribu kati ya wawili hao na kusema anataka kuona urafiki huo ukififia. “Inashangaza kuwa huyo mlofa anataka kushinda na mume wangu mchana kutwa kila siku. Ni kama hajui mpenzi wangu sharti aniweke mstari wa mbele kwa kunipa muda wote kwa kuninong’onezea ya mahaba,” mrembo alitamka kwa hasira.

Tetesi hizo zilipomfikia kalameni, alicheka na kusema atapuuzilia mbali mawazo kama hayo. “Sitakoma kuenda kwa rafiki yangu na hata kukesha huko. Chake ni changu, na changu ni chake. Mkewe hana budi ila kuzidi kunipikia bila kuchoka ili tujue ni mke mwema au la,” kalameni alisema mtaani.

Hata hivyo, mambo yalienda kombo juzi kalameni alipofika kwa rafiki yake hata kabla ya wenyewe kutoka kitandani. Wawili hao walitoka chumba cha kulala, mgeni wao alipowaita kwa sauti ya juu. “Yaani mnalala hadi saa mbili ya asubuhi? Hata kama ni wikendi hamfai kulala sana,” kalameni alisema na kucheka ovyo.

Mara mmoja mrembo alimfokea kwa kuwasumbua wakiponda raha na kumtaka awakome kabisa.

Kilichofuata kikawa majibizano makali hadi kalameni akaoondoka akiwa ameaibika mno.