Kalonzo achanganyikiwa baada ya kutoka Azimio, ataka muda wa kutafakari

Kalonzo achanganyikiwa baada ya kutoka Azimio, ataka muda wa kutafakari

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka ameonakana kuchanganyikiwa aliposema bado ana nafasi ya kurejea ndani ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya baada ya kutangaza kujiondoa na kuwania urais kwa tiketi ya chama chake.

Akiongea na wanahabari jijini Nairobi wakati ambapo mgombea wa urais wa Azimio Raila Odinga alitangaza kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake, Bw Musyoka alisema atanyamaza kwa muda kutafakari kuhusu matukio ya siasa nchini.

“Nitanyamaza kwa kipindi cha wiki moja ili kuwazia matukio ya leo. Lakini leo (jana Jumatatu) tumeamua kujitenga kwa ajili ya mustakabali wa taifa hili. Hata hivyo, sitakuwa nimechelewa kwa sababu ninaweza kurejea nyumbani tena,” Bw Musyoka akasema.

Ingawa kiongozi huyo wa Wiper alitangaza kujiondoa kutoka Azimio, Bw Odinga alimteua kuwa Mkuu wa Mawaziri endapo atashinda katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Kando na Bw Musyoka, wengine waliopewa nyadhifa ni Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho alitengewa Wizara ya Ardhi, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alitengewa Wizara ya Fedha huku Waziri wa Kilimo Peter Munya akitengewa wizara hiyo hiyo, endapo Bw Odinga atabuni serikali ijayo.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anasema kuwa huenda Bw Musyoka anataka kutumia muda huo wa wiki moja kukadiria ikiwa hatua yake ya kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais itaweza kusababisha kukosekana kwa mshindi wa moja kwa moja katika kinyang’anyiro cha urais.

“Ikiwa Kalonzo atashawishika kuwa akiwania urais William Ruto na Raila Odinga watakosa kupata asilimia 50 na kura moja basi hatarudi nyuma. Lakini akigundua kuwa hataweza kuwakosesha wawili hao ushindi wa moja kwa moja basi huenda akachukua wadhifa aliopewa na Raila,” akasema Bw Andati.

Bw Kalonzo na wafuasi wake wamekuwa wakishikilia kuwa endapo Bw Odinga hatamteua kuwa mgombea mwenza wake, itakuwa vigumu kwa kiongozi huyo wa ODM kupata ushindi.

“Ningependa kumhakikishia ndugu yangu Raila kwamba endapo anataka kupata ushindi katika uchaguzi mkuu ujao basi hana budi kuniteua kuwa mgombea mwenza wake. Sifai kufanyiwa mahojiano kwa sababu nimewahi kuwa mgombea mwenza wake mara mbili kando na kuwahi kuhudumu kama Makamu wa Rais chini ya utawala wa Hayati Mwai Kibaki,” akasema wiki jana katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos.

Bw Musyoka anaonekana kutegemea kura 1.6 milioni za eneo la Ukambani kuweza kuvuruga hesabu za Dkt Ruto na Bw Odinga katika eneo la Ukambani.

Isitoshe, wandani wake wanasema kuwa kiongozi huyo ana uwezo wa kuvutia zaidi ya kura 1.9 milioni kutoka sehemu nyingine za nchini ambako kuna wafuasi wake.

Itakumbukwa kwamba alipowania urais kwa mara ya kwanza mnamo 2007 Bw Musyoka alipata kura 879,903 alipowania urais kwa mara ya kwanza kwa tiketi ya chama cha ODM-Kenya.

Hii ni baada ya kutengena na Bw Odinga ambaye aliwania urais kwa tiketi ya chama cha ODM na kuwa wa pili kwa kupata kura 4,352,993 nyuma ya Kibaki aliyetangazwa mshindi kwa kupata kura 4,584,721.

Hii ina maana kuwa endapo Bw Musyoka asingetengana na Bw Odinga, kiongozi huyo wa ODM angemshinda Rais Kibaki katika uchaguzi huo, ambao matokeo yake yalisababisha utata.

You can share this post!

Raila ajaribu kumzima Ruto kwa ahadi za vyeo

Nazlin Umar amteua naibu mwenye umri wa miaka 26

T L