Habari MsetoSiasa

Kalonzo ahusishwa na mauaji ya mtu katika mzozo wa ardhi

November 12th, 2019 1 min read

Na CHARLES WANYORO

MSHUKIWA wa mauaji kutoka kijiji cha Kianda, Igembe Kusini, Kaunti ya Meru anataka Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka aandikishe taarifa kwa polisi kuhusu zogo la ardhi lililosababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wengi kujeruhiwa mwezi uliopita eneo hilo.

Bw Joseph King’ori M’ikamati amemshutumu Bw Musyoka kwa kutumia ushawishi wake kuvuruga uchunguzi kuhusiana na mzozo huo wa ekari 2,000 za ardhi katika eneo la Amung’enti ‘D’ kwa maslahi yake mwenyewe.

Mshukiwa huyo anadai kwamba ardhi hiyo inamilikiwa na koo tano za jamii ya Ameru wala si Bw Musyoka anayedaiwa kuimiliki kupitia washirika wake.

Kupitia wakili wake, Bw Kirimi Mbogo, mshukiwa huyo anataka Bw Musyoka awajibikie kifo cha marehemu George Mithika ambaye aliaga dunia kwenye ghasia zilizotokea Oktoba 4, 2019 kuhusu kipande hicho cha ardhi.

Aidha, alieleza Jaji wa Meru Alfred Mabeya kwamba anaamini Bw Musyoka amekuwa akiwasiliana na Kamashina wa Meru, Bw Allan Machari, Naibu Kamishina wa Igembe Kusuni, Bw James Koskey na maafisa wengi wa vyeo vya juu kuhusu utata huo akilenga kujinufaisha na ardhi hiyo.

Vilevile alieleza mahakama kuwa kabla ya kutokea kwa ghasia zilizosababisha mauaji hayo, makundi yanayomuunga mkono Bw Musyoka yalikutana katika vituo vya polisi vya Nthanjene na Tumu Tumu ambako walikula kiapo kinachowaunganisha katika kuwatimua wakulima wote wanaoishi kwenye ardhi hiyo.