Kalonzo amponda Ruto kwa kupinga wazo la urais wa mzunguko

Kalonzo amponda Ruto kwa kupinga wazo la urais wa mzunguko

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka ndiye kiongozi wa hivi punde kuunga mkono pendekezo la Rais Uhuru Kenyatta kwamba jamii zingine, isipokuwa Wakikuyu na Wakalenjin, zinapasa kupewa nafasi kuliongoza taifa hili 2022.

Akiongea Jumatano alipoongoza hafla fupi ya kumzindua mgombeaji wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos Agnes Kavindu Muthama, Bw Kalonzo alisema ni unafiki mkubwa kwa Naibu Rais William Ruto kupinga wazo hilo ilhali limewahi kuibuliwa na mwandani wake, Johntone Muthama.

Bw Musyoka pia alimkosoa Dkt Ruto kwa kudai pendekezo hilo linaendeleza ukabila ilhali yeye (Ruto) hajawahi kupendekeza uteuzi wa watu kutoka makabila mengine katika serikali hii ya Jubilee.

“Ni unafiki kwamba Ruto anapinga wazo hili zuri kutoka kwa Rais Kenyatta ilhali mheshimiwa Muthama ambaye ni rafiki yake sasa ndiye alitoa pendekezo hilo mwanzoni. Isitoshe, yeye mwenyewe alidhihirisha ukabila kati ya 2013 na 2017 wakati aligawana serikali nusu bin nusu na Rais Kenyatta,” akawaambia wanahabari.

Akaongeza: “Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta alitoa kauli yenye mashiko aliposema kuwa Kenya ni taifa lenye jamii 43 ambazo zote zina haki ya kuongoza wala sio jamii mbili pekee ambazo zimetuongoza tangu uhuru 1963. Kwa hivyo, ni unafiki kwa Naibu Rais kupinga kauli hiyo na kudai anatetea Kenya isiyo na ukabila ilhali amekuwa akiendeleza ukabila huo tangu Jubilee ilipoingia mamlakani 2013,”

Bw Musyoka alidai kuwa Dkt Ruto alitumia asilimia 50 ya usemi aliyopewa katika serikali ya muungano wa Jubilee mnamo 2013 kuteua watu kutoka jamii yake pekee, tofauti na Rais Kenyatta.

“Sasa ni wazi Rasis Kenyatta ni kiongozi asiyeongozwa na ukabila wala sio Ruto ambaye sasa atakuja katika kaunti ya Machakos kuwahadaa watu wetu kwa pesa ambazo zimepatikana kwa njia zisizo za ukweli. Ikiwa kweli anapenda watu wetu wa Ukambani mbona hakutupa hata nafasi moja ya uwaziri katika serikali ya Jubilee 2013?,” akauliza.

Wakati huo huo, Bw Musyoka alifafanua kuwa chama cha Wiper hakijaongozwa na nia ya kuvunja familia kwa Bi Kavindu kwa kuamua kumpokeza tiketi yake katika uchaguzi huo mdogo wa useneta wa Machakos.

Alieleza kuwa Wiper ilizingatia tajriba na sifa za uongozi wa mwanasiasa huyo wala sio uhusiano wake wa kifamilia. Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa seneta wa Machakos Boniface Mutinda Kabaka.

Bi Kavindu ni mke, aliyetengana, wa Seneta wa zamani wa Machakos Johnstone Muthama ambaye ndiye mshirika mkuu wa Naibu Rais William Ruto kutoka eneo la Ukambana. Bw Muthama ambaye ni kiongozi wa chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA), ametangaza kuwa chama hicho kitadhamini mgombeaji katika uchaguzi huo mdogo.

“Tumemteua Bi Kavindu kwa sababu ni kiongozi mwenye sifa zinazolandama na sera zetu kama chama cha Wiper. Ni kiongozi mwadilifu ndio maana Rais Uhuru Kenyatta alimteua kama mwanachama wa Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI) na mwanachama wa Bodi ya Kampuni ya Maji ya Tana Athi. Hatukuongozwa na nia ya kuvuruga familia ya rafiki yetu wa zamani,” Bw Musyoka akawaambia wanahabari katika makao ya Wiper, Karen, Nairobi.

Mgombeaji wa Wiper katika uchaguzi mdogo wa wadi wa Kitise/Kithuke, Makueni Sebastian Muli Munguti pia alikabidhiwa cheti cha uteuzi na mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya Wiper Bi Agatha Solitei.

Bi Kavindu alipata idhini ya kupeperusha bendera ya Wiper katika uchaguzi huo mdogo wa useneta baada ya watu wengine waliotaka tiketi hiyo kujiondoa na kuapa kumuunga mkono. Wao ni aliyek,uwa Mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile, Mshirikishi wa kampeni za BBI Ukambani Jackson Kala na mjane wa marehemu Kabaka Bi Jeniffer Mutinda.

Bi Kavindu ambaye aliwania kiti cha Mwakilishi wa Wanawake Machakos kwa tiketi ya Jubilee katika uchaguzi wa 2017 alisema kuwa alihamia Wiper kwa idhini ya Rais Kenyatta.

“Nilihamia Wiper kwa idhini ya kiongozi wa Jubilee Rais Kenyatta na nitasalia hapa kwa baraka za kiongozi wetu Stephen Kalonzi Musyoka,” akasema huku akielezea nia ya kushinda katika uchaguzi huo wa Machi 18.

Tayari Chama cha Maendeleo Chap Chap (CCM) chake Gavana Alfred Mutua tayari kimemteua aliyekuwa Waziri wa Maji na Mbunge wa Mwala Mutua Katuku kuwa mgombeaji wake. Nacho chama cha UDA kinapania kuteua aliyekuwa Naibu Gavana wa Machakos Benard Kiala.

Hafla hiyo ya uzinduzi wa Bi Kavindu ilihudhuriwa na viongozi katika wa Wiper. Miongoni mwao ni Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Wavinya Ndeti, Naibu Katibu Mkuu Peter Mathuki, Mbunge Mwakilishi wa Machakos Joyce Kamene na wabunge Patrick Makua (Mavoko) na Daniel Maanzo.

You can share this post!

Polisi akana kumuua mwenzake kituoni

Maajabu ya pacha kufariki siku moja