Kalonzo arai Raila awe mgombea mwenza wake uchaguzini 2022

Kalonzo arai Raila awe mgombea mwenza wake uchaguzini 2022

Na ANTHONY KITIMO

KIONGOZI wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, amesifia hatua ya ODM kujiondoa katika muungano wa NASA na akamuomba kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga, kujiunga naye kama mgombea-mwenza kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Akihutubu katika eneo la Akamba Handicraft, Changamwe, Kaunti ya Mombasa, Bw Musyoka alisema hatua ya ODM kusema itaondoka NASA inaashiria mwisho wa muungano huo.

Alisema vyama hivyo sasa vinapaswa kuungana kukabili wale wanaohusishwa na tuhuma za ufisadi licha ya kukumbwa na sakata za ufisadi.

“Ninamshukuru ndugu yangu mkubwa Raila. Nimemuunga mkono kikamilifu kwa zaidi ya miaka 10. Ninachosema ni kuwa hakuna deni lolote la kisiasa japo ningemtaka kujiunga nami kama mgombea-mwenza ili kuiwezesha nchi hii kuendelea mbele,” akasema Bw Musyoka.

Akaongeza, “Wakati huu, nitakuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu Agosti ijayo. Sitaki kuonekana kama mwaniaji dhaifu tena kwa kisingizio cha kurejesha amani nchini.”

Akihutubu siku moja baada ya ODM kutangaza kujindoa NASA na kuanza safari mpya ya kisiasa, Bw Musyoka alisema Wiper inaamini kuwa Bw Odinga atajiunga na OKA.

You can share this post!

Kaunti 10 za Mt Kenya kuondoa ada za biashara

MAKALA MAALUM: Kero ya wakazi kugeuza makaburi ya umma...