Kalonzo atarajiwa tena Azimio

Kalonzo atarajiwa tena Azimio

NA PIUS MAUNDU

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka alikuwa ameamua kujiunga na kampeni za kumpigia debe mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga hata kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumzima kuwania urais, naibu mwenyekiti wa chama hicho Mutula Kilonzo Junior amesema.

Mnamo Ijumaa, IEBC ilimzuia Bw Musyoka kuwania urais kwa sababu hakuwa amewasilisha orodha ya watu wanaoidhinisha azma yake, kwa mfumo wa “Microsoft Excel sheet” inavyotakikana.

Bw Kilonzo Junior aliungana na viongozi wa Wiper ambao wiki jana walimwekea presha kiongozi huyo arejee Azimio baada ya kutangaza kujiondoa mnamo Mei 15, 2022.

Makamu rais huyo wa zamani alitangaza kuwa alijitosa katika kinyanga’anyiro cha urais kwa kukosa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.Nafasi hiyo ilimwendea kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua.

Bw Musyoka alimteua aliyekuwa mgombea kiti cha useneta wa Narok kwa tikiti ya Wiper Andrew Sunkuli kuwa mgombea mwenza wake.

Kilonzo Junior ni miongoni mwa kundi la viongozi wa Wiper ambao wamekuwa wakimshinikiza Bw Musyoka atengane na Bw Odinga na awanie urais kivyake.

Hata hivyo, Jumamosi alijiondolea lawama akisema kwamba yeye ni miongoni mwa viongozi waliomshinikiza kiongozi huyo wa Wiper ajiondoe Azimio.

“Bw Musyoka aliamua kivyake kujiondoa kulalamikia ‘dhuluma’ zilizochangia kutoteuliwa kwake kuwa naibu wa Bw Odinga na kudumisha heshima ya jamii ya Wakamba,” Seneta huyo wa Makueni akasema.

Hata hivyo, akaeleza, Bw Musyoka alibadili msimamo wake na akawashauri wandani wake kuunga mkono azma ya Bw Odinga.

“Bw Musyoka alituambia tuitishe mkutano na tutangaze kuwa ameamua kufanya kazi na wale ambao wanalenga kuendeleza amani nchini na kukomesha ufisadi,” Kilonzo Junior alisema katika mkutano wa kampeni eneo la Kisau, kaunti ya Makueni Ijumaa.

“Ingawa tumedhulumiwa, tutafanya kazi na hawa watu,” akaongeza, akifichua kuwa Bw Musyoka anafanya mazungumzo na uongozi wa muungano wa Azimio.

Habari kwamba Bw Musyoka yu njiani kurejea Azimio ziliibua tumbojoto miongoni mwa wandani wa Bw Odinga kutoka eneo la Ukambani.

Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana ambaye anaongoza kundi lililotwikwa jukumu ya kuendesha kampeni za mgombea urais huyo wa Azimio katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni alisema kuwa wandani wa Odinga katika eneo hilo pia sharti washirikishwe katika mazungumzo kati ya Bw Musyoka na uongozi wa Azimio.

Ingawa wako na matumaini ya kuvutia sehemu kubwa ya kura 1.6 milioni za eneo hilo katika kapu la Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, wanaungama kuwa uwepo wa Bw Musyoka utarahisisha kazi yao.Lakini wameingiwa na wasiwasi kwamba Bw Musyoka anapanga kuwasukuma nje ya Azimio.

“Hatimaye Wiper imeamua kujiunga na Azimio ambako jamii ya Wakamba wamo, miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu. Mazungumzo na uongozi wa Azimio sharti yatushirikishe sisi ambao tumekuwa tukiuza muungano huo Ukambani. Tunataka haki na ungwana,” Profesa Kibwana akasema katika taarifa iliyowakera wandani wa Bw Musyoka.

  • Tags

You can share this post!

Walimu wataka vyumba vya kunyonyeshea vijengwe shuleni

Gachagua apotezea Kenya Kwanza kura

T L