Habari Mseto

Kalonzo atetea Uhuru kukopa mabilioni

October 1st, 2020 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

KINARA wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ametetea hatua ya serikali kuendelea kuchukua mIkopo kutoka nchi za nje licha ya deni la taifa kufikia kiwango cha kutisha cha Sh6.6 trilioni.

Bw Musyoka alisema fedha zinazokopwa zitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali na kuisaidia serikali kutimiza ajenda zake nne kuu.

Kati ya miradi ambayo Bw Musyoka aliitaja ni ujenzi na uimarishaji wa miundomsingi itakayosaidia kukuza uchumi wa nchi hii.Kauli ya Bw Musyoka ilijiri wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta ameelekea Ufaransa kutia saini mkopo wa kufadhili miradi ya ujenzi wa barabara unaokisiwa kuwa mabilioni ya fedha.

Akitetea ziara ya Rais Kenyatta Ufaransa na mikopo iliyotolewa kwa nchi, Bw Musyoka ambaye chama chake kimeingia ushirikiano na Jubilee, alisisitiza kwamba hela zilizokopwa miaka ya nyuma zimesaidia taifa kujiendeleza kiuchumi.

“Tumeona miradi mingi ambayo imetekelezwa nchini ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na miradi mingine ya ujenzi wa barabara Nairobi na maeneo mengine. Miradi iliyotekelezwa ina umuhimu sana kwa kuimarisha uchumi wa nchi,” akasema akizungumza na wanahabari mjini Wundanyi.

Kenya imekuwa ikichukua mikopo ya mabilioni ya fedha hasa kutoka China, hali ambayo imezua wasiwasi kwamba huenda taifa likazama kwenye lindi la deni na kushindwa kujikwamua.

“Sidhani kwamba Ukoloni wa China utatimia nchini kwa sababu ya madeni haya. Kile ambacho tunahitaji ni serikali kujadiliana upya na kurefusha muda unaofaa kuilipa,” akaongeza.

Baadhi ya viongozi wamekuwa wakikashifu Rais Kenyatta kwa kukopa hela nyingi huku sehemu ya pesa ikiporwa na miradi iliyolengwa kukosa kukamilika.

Bw Musyoka ambaye amekuwa katika ziara ya kujivumisha Pwani, tangu wikendi jana aliandaa misururu ya mikutano katika Kaunti ya Taita Taveta. Aliandamana na mwenyekiti wa Wiper Chirau Mwakere, Naibu Gavana Majala Mlaghui, mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako na viongozi wengine wa chama hicho.