Kalonzo avua kivuli cha Raila

Kalonzo avua kivuli cha Raila

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka hatimaye ameonekana kujitoa kwenye kivuli cha kiongozi wa ODM, Raila Odinga baada ya chama hicho kutangaza jana kuondoka rasmi katika muungano wa NASA.

Muungano huo ambao umehusishwa na Bw Odinga, sasa utasalia na vyama vinne; Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Musalia Mudavadi, Ford Kenya chake Moses Wetang’ula, ODM na Chama cha Mashinani (CCM) cha aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto.

“Chama cha Wiper kimeamua kujiondoa NASA na sasa tutaanza kufanya mazungumzo na vyama vingine kwa lengo la kuunda muungano mpya na hatimaye kuunda serikali ijayo,” akasema Bw Musyoka baada ya mkutano uliofanyika katika makao makuu ya Wipet mtaani Karen, Nairobi.

Bw Musyoka alisisitiza kuwa hatakuwa mwaniaji mwenza wa mwanasiasa yeyote katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Gavana wa Kitui, Charity Ngilu tayari ameonya vinara wa NASA kuwa, watabwagwa na Naibu wa Rais William Ruto mwaka ujao iwapo watatengana.

Kulingana na mkataba wa maelewano, muungano wa NASA utavunjika iwapo vyama visivyopungua vitatu vitajiondoa.

Alhamisi iliyopita, Naibu Kiongozi wa ANC, Ayub Savula alitangaza kuwa chama hicho kimemwandikia barua Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Ann Nderitu kikitaka kujiondoa NASA.

Lakini Nderitu alisema Jumatatu kuwa hajapokea barua kutoka kwa chama chochote kikitaka kujiondoa NASA.

Bi Nderitu alisema kuwa, hata chama cha CCM kiko ndani ya NASA licha ya kutangaza kuwa kitaunga Naibu wa Rais William Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Bi Nderitu tayari ameonya Ford Kenya kuwa hakiwezi kujiondoa kutoka ndani ya NASA hadi pale mzozo wa uongozi wa chama hicho utakapotatuliwa.

Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula na mbunge wa Kanduyi, Wafula Wamunyinyi wamekuwa wakipigania uongozi wa Ford Kenya na kesi hiyo iko kortini.

Bw Wetang’ula ametaja kundi la Bw Wamunyinyi kuwa waasi ambao wanalenga kuvuruga chama.

Bw Odinga jana Jumatatu alikimbia kutuliza joto ndani ya Wiper kwa kuwahakikishia kuwa atagawana na vyama vilivyo ndani ya muungano wa NASA fedha ambazo ODM ilipokea kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa.

Fedha hizo zimesababisha mvutano mkubwa kati ya viongozi wa ODM na Wiper.

“Leo (Jumatatu) nimepokea barua iliyotiwa saini na Bw Odinga mwenyewe ambapo alituhakishia kuwa tutapata sehemu ya mgao wa fedha ambazo ODM ilipokea kutoka Hazina ya Vyama vya Kisiasa,” akasema Bw Musyoka.

Bw Musyoka alisema atapeleka barua hiyo kwa Bi Nderitu kama ushahidi wa kuonyesha kwamba ODM itatoa mgao wa fedha hizo kwa Wiper.

Hazina ya Kitaifa imetenga jumla ya Sh516 milioni kwa ajili ya chama cha Jubilee na ODM katika bajeti ya mwaka huu wa fedha. Chama cha ODM kitapokea Sh165 milioni.

Katika bajeti ya mwaka uliopita, vyama hivyo viwili vilipokea jumla ya Sh830 milioni; ambapo ODM ilipokea Sh260 milioni.

Fedha hizo hutolewa kwa kuzingatia kura ambazo chama cha kisiasa kilipata katika kinyang’anyiro cha urais.

You can share this post!

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Kiambu washauriwa...

Niko tayari kutetea taji langu la marathon Olimpiki –...