Kalonzo awalilia vinara wa OKA wampe tiketi apeperushe bendera ya urais 2022

Kalonzo awalilia vinara wa OKA wampe tiketi apeperushe bendera ya urais 2022

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amewalilia vinara wenza katika Okoa Kenya Alliance (OKA) kumpa tiketi ya muungano huo kupeperusha bendera ya urais uchaguzi mkuu ujao.

OKA inajumuisha Mabw Kalonzo, Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetangula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (KANU).

Huku Bw Moi na ambaye ni seneta wa Baringo Alhamisi akitangaza azma yake kuwania urais 2022, Kalonzo amewahimiza vinara wenza katika OKA kumpa tiketi ya urais akihoji yeye ndiye tiba ya changamoto zinazozingira Wakenya.

“Muniombee niteuliwe kupeperusha bendera ya OKA kugombea urais. Nikiteuliwa tutafanya kazi pamoja na ndugu yangu Gideon Moi,” Bw Kalonzo akasema, akizungumza katika kongamano la KANU, Ukumbi wa Bomas, jijini Nairobi.

“Haya mambo mtuachie, mimi na Gideon,” kiongozi huyo wa Wiper akaonekana kurai vinara wenza katika OKA, akielezea uhusiano wake wa karibu na Rais wa zamani Daniel Arap Moi ambaye kwa sasa ni marehemu.

Mabw Raila Odinga (ODM), Mudavadi, Wetangula, na Isaac Ruto (Chama Cha Mashinani) ni kati ya wageni mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo ya KANU.

Bw Odinga na Bw Mudavadi pia wameashiria kugombea urais 2022, kumrithi Rais Uhuru Kenyatta huku Naibu Rais Dkt William Ruto akiendeleza kampeni kusaka kura kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya.

You can share this post!

Kanini Kega abadili kauli ya kumuunga Raila 2022, asema...

West Ham kukosa wanasoka wawili tegemeo dhidi ya Rapid...