Habari MsetoSiasa

Kalonzo azidi kutengwa na viongozi Ukambani

November 4th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MASAIBU ya Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kutengwa na viongozi katika ngome yake ya Ukambani yalizidi wikendi, magavana watatu wa eneo hilo, walipotofautiana naye kuhusu uchaguzi mdogo wa Kibra.

Magavana hao Charity Ngilu (Kitui), Prof Kivutha Kibwana(Makueni) na Dkt Alfred Mutua(Machakos), walijiunga wazi na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kumpigia debe Bw Bernard Okoth.

“Kibera inahitaji kiongozi shupavu na sisi tuna imani kwamba Imran anajali maslahi ya watu wa Kibra jinsi alivyokuwa nduguye marehemu Ken Okoth,” akasema Dkt Mutua walipokutana na Bw Odinga

Chama cha Wiper kilitangaza kwamba kinamuunga mkono mwaniaji wa Ford Kenya, Bw Khamisi Butichi.

Jana, Bi Ngilu, Dkt Mutua na Prof Kibwana, waliendeleza kampeni tena na Bw Odinga katika mkutano mkubwa wa kisiasa uwanja wa Joseph Kangethe, kumpigia Bw Okoth debe kabla ya uchaguzi huo, unaoandaliwa Alhamisi wiki hii.

Hatua hii inajiri muda mfupu baada ya baada ya chama cha Maendeleo Chap Chap(MCC) kinachoongozwa na Dkt Mutua kushinda kiti cha udiwani cha Mutonguni.

Madiwani wa Kaunti ya Makueni nao wamekuwa wakimkaidi Bw Musyoka na kuunga mkono sera za uongozi za Prof Kibwana.