Kalonzo azindua sekretarieti ya kushirikisha kampeni zake za urais

Kalonzo azindua sekretarieti ya kushirikisha kampeni zake za urais

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka Jumatatu, Agosti 9, 2021 alizindua nguzo tano ambazo zitahimili azma yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Akiongea alipozindua sekretarieti itakayoshirikisha kampeni zake za urais, SKM Command Centre, eneo la Karen, Nairobi, Bw Musyoka alisema hata hivyo kampeni zake zitajikita zaidi katika ufufuzi wa kiuchumi na maendeleo endelevu.

Vile vile, makamu huyo wa rais wa zamani alitaja kilimo cha kiasili, vita dhidi ya ufisadi, udhibiti wa madeni na uwezeshwaji wa vijana na wanawake katika sera ambazo ataendeleza endapo atachaguliwa kuwa rais mnamo Agosti 9, 2022.

“Nguzo hizi zitajenga azimio langu ambalo litaandaliwa na kituo cha SKM Command Centre, ambacho tumezindua leo (jana Jumatatu). Azimio hilo litazinduliwa kwa wananchi katika miezi ijayo ili Wakenya waweze kulichambua na kulielewa,” Bw Musyoka akasema.

Alieleza kuwa utawala wale utatoa kipaumbele kwa uwekezaji katika miradi ya kuongeza thamani bidhaa za kilimo, kulainisha mfumo wa utozaji ushuru, utoaji wa ruzuku na soko kwa mazao ya wakulima.

“Vile vile, tutaanzisha vita vikali dhidi ya ufisadi katika sekta ya umma na kujenga miundombinu ambayo itasaidia kuleta faida kwa biashara na aina nyingine za uwekezaji,” akasema Bw Musyoka.

Ili kupunguza misongomano katika miji mikuu nchini, kiongozi huyo wa Wiper alisema serikali yake itawekeza katika mabasi makubwa ya uchukuzi wa umma.

Bw Kalonzo hakuchelea kushambulia mpango wa kiuchumi unaovumishwa na Naibu Rais William Ruto wa kuchochea uchumi kuanzia chini yaani “bottom up economic model” na kauli mbiu ya hasla akisema hiyo sio suluhu ya kudumu kwa changamoto zinazosibu taifa hili.

“Hiyo ni suluhu ya muda tu. Hawa ni viongozi ambao wanajaribu kutumia mahangaiko yetu kwa manufaa yao ya kisiasa. Ni vipi mtu atapendekeza mfumo wa kiuchumi ambao hauakisi safari yake maisha. Tunapaswa kuchambua matatizo yanayoathiri Kenya na kubuni miongozo ambayo itaweze kufanya kazi,” Bw Musyoka akasema.

Kiongozi wa Wiper pia alisema atabadili mfumo wa utozaji ushuru katika sekta ya mafuta na gesi kwa lengo la kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu.

“Hii ndiyo njia ya kipekee ya kupunguza gharama ya uendeshaji wa biashara na kuongeza faida itokanayo na shughuli hizo,” akasema.

Wakati huo huo, Bw Musyoka alielezea matumaini kuwa kama wanachama wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) yeye na vinara wenzake watasalia pamoja ili kufikia lengo lao la “kukomboa taifa hili mwaka 2022.”

Vinara wengine wa muungano huo ni Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi ambaye hata hivyo ameapa kutojiondoa kwenye muungano kati ya chama chake, KANU, na chama tawala, Jubilee.

Bw Mudavadi alihudhuria shughuli hiyo lakini Bw Wetang’ula aliwakilishwa na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa.

Naye Bw Moi aliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kanu George Wainaina.

Bw Mudavadi pia alisema kuwa wao kama vinara wa OKA wataendelea kuungana “kwa manufaa ya taifa hili”.

You can share this post!

Ruto akita kambi Nakuru kupigia debe mfumo wa kumuinua...

Wanjigi avamia Mlimani kusaka kura za urais