Kalonzo, Gideon sasa njia panda kisiasa baada ya OKA kusambaratika

Kalonzo, Gideon sasa njia panda kisiasa baada ya OKA kusambaratika

WANDERI KAMAU na RUTH MBULA

KIONGOZI wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka na mwenzake wa Kanu, Bw Gideon Moi, sasa wako kwenye njia panda kisiasa baada ya kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi kutangaza azma ya kuwania urais jana Jumapili.

Hatua ya Bw Mudavadi jana pia inafasiriwa kama ishara ya kusambaratika rasmi kwa muungano wa Okoa Kenya Alliance (OKA) ambao umekuwa ukiwashirikisha vigogo hao watatu na kiongozi wa Ford-Kenya, Seneta Moses Wetang’ula (Bungoma).

Bw Wetang’ula pia ni miongoni mwa viongozi waliotangaza “kwenda safari moja ya kisiasa” na Bw Mudavadi, akimsifia kuwa “ndugu yake wa muda mrefu.”

Kwenye hotuba yake kwenye hafla hiyo, Naibu Rais William Ruto alitangaza kubuni ushirikiano kati ya chama chake cha UDA, ANC na Ford-Kenya.

Wadadisi wa siasa wanasema ikizingatiwa sasa ni rasmi Bw Mudavadi ameungana na Dkt Ruto ielekeapo Agosti, ni wazi Mabwana Kalonzo na Gideon lazima wafanye maamuzi muhimu ya kisiasa kwa haraka ili kutoendelea kubaki gizani.

Jumapili, wawili hao walionekana kuchanganyikiwa, kwani walilazimika kuondoka ghafla katika Ukumbi wa Bomas, walipobaini Dkt Ruto alikuwa miongoni mwa vigogo wa kisiasa ambao wangehudhuria hafla hiyo.

Baadaye, viongozi hao waliwaita kuwahutubia wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi, lakini wakabadilisha mipango yao ghafla.

Baada ya kufanya kikao cha faragha kwa dakika chache, waliondoka kwa haraka bila kuwahutubia.

Hata hivyo, Katibu wa Masuala ya Kisiasa katika Kanu, Bw Fredrick Okango, alisema kuwa Mabwana Kalonzo na Gideon waliondoka katika hafla hiyo “kama ishara ya hekima.”

“Tuliamua kuondoka katika hafla ya Bw Mudavadi bila nia yoyote mbaya. Tuliheshimu mwaliko wake kuhudhuria uzinduzi wa azma yake ya urais lakini tukaondoka baada ya watu ambao hatukuwatarajia kuhudhuria pia. Baadhi ya marafiki wake si marafiki wetu na tulihisi kutokuwa salama tukiwa katika mazingira sawa. Tunamtakia kila la heri anapotafuta ushirikiano na washirika wengine wa kisiasa,” akasema Bw Okango kwa niaba ya viongozi hao.

Gavana wa Kisii, Amos Nyaribo, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Mudavadi, alisema hataungana naye kwenye ushirikiano wake mpya na Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Ruto apasua OKA

WANDERI KAMAU: Tubadilishe taratibu za kuwachagua magavana

T L