Kalonzo kimya ngome yake ikivamiwa

Kalonzo kimya ngome yake ikivamiwa

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI WA WIPER Kalonzo Musyoka ameonekana kulegea huku Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wakivamia ngome yake ya Ukambani kusaka kura za 2022.

Dkt Ruto na Bw Odinga ndio wapinzani wakuu wa Bw Musyoka ambaye pia anasaka tiketi ya kuwania urais chini ya mwavuli wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Mnamo Ijumaa, Dkt Ruto alirejea kwa mara ya tano katika eneo la Ukambani kuendesha kampeni katika vituo mbali mbali katika maeneo bunge ya Kitui Mashariki na Kitui Kusini. Naibu Rais alivumisha chama chake, United Demokratic Alliance (UDA) na mpango wake wa ukuzaji uchumi kuanzia mashinani, almaarufu “Bottom-Up economic model”.

Naye Bw Odinga alipele – ka kampeni yake ya Azimio la Umoja katika Kaunti ya Makueni ambapo alikutana na magavana watatu kutoka Ukambani, madiwani, wafanyabiashara na viongozi wa mashinani kabla ya kuhutubia mkutano mkubwa mjini Wote.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyosomwa na Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua, kwa niaba ya Profesa Kivutha Kibwana (Makueni) na Charity Ngilu (Kitui), magavana hao walimlaumu Bw Musyoka kwa kuchangia ukosefu wa maendeleo katika eneo hilo kwa miaka mingi. Walidai kiongozi huyo wa Wiper amekuwa akiendeleza maslahi yake binafsi badala ya yale ya wananchi.

“Tumejadiliana kuhusu changamoto zinazokabili eneo letu kama vile ukosefu wa nafasi za kiuchumi, ukame wa kila mara, ukosefu wa masoko, ubovu wa miundo msingi, ukosefu wa usalama, kuko – sa ajira, umasikini miongoni mwa zingine. Hizi ni shida ambazo Kalonzo ameshindwa kushughulikia licha ya kushikilia nyadhifa kubwa serikalini tangu 1983,” akasema Dkt Mutua.

Akaongeza: “Hii ndio maana sasa tumeamua kumuunga mkono Raila kuwa Rais na tunaunga ajenda yake ya umoja, ustawi na ushirikishwaji wa wote inayoendelezwa kupitia kauli mbiu ya Azimio la Umoja.”

Dkt Ruto anaonekana kupata nafasi na nguvu ya kuendesha kampeni katika eneo la Ukambani baada ya mgombeaji wa chama cha Wiper kubwagwa katika uchaguzi mdogo katika wadi ya Nguu/ Masumba, Kaunti ya Makueni.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 18, 2021, mgombeaji huyo Eshio Maundu Mwaiwa, alishika nambari tatu ambapo mgombeaji huru Timothi Maneno aliibuka mshindi.

Mgombeaji wa chama cha UDA Daniel Musau alikuwa wa pili katika kinyang’anyiro hicho, matokeo ambayo yalimchangamsha Dkt Ruto na wandani wake katika vuguvugu la “The Hustler Nation” ikizingatiwa kuwa hiyo ni ngome ya Bw Musyoka.

Wadadisi sasa wanahisi kuwa Bw Musyoka amelegea kwa kuwa hajawahi kurejea katika eneo hilo wala kuitisha mkutano wa viongozi wa Wiper kutoka eneo hilo, alivyoahidi, ili kutathmini kiini cha kushindwa kwa mgombeaji wa Wiper.

 

You can share this post!

Kinaya Ruto akiita mawaziri wanaomkosoa

Rais Odinga: Mwanzo mpya au ahadi hewa?

T L