Kalonzo, Kivutha waahidi kushirikiana katika maendeleo

Kalonzo, Kivutha waahidi kushirikiana katika maendeleo

BENSON MATHEKA NA PSCU

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana, wamesema kwamba hawatakubali tofauti za kisiasa zivuruge miradi ya maendeleo ambayo serikali imeanzisha eneo hilo.

Viongozi hao walimwambia Rais Uhuru Kenyatta kwamba tofauti na inavyodaiwa, viongozi wa eneo la Ukambani hawajagawanyika na wanashirikiana pamoja kuimarisha maisha ya wakazi.

“Tunashukuru kwamba umekuja kuzindua na kukagua miradi katika eneo letu. Tunakuhakikishia kwamba hakuna siasa za pesa nane zitavuruga miradi hii. Tumeungana kama viongozi,” Gavana Kibwana akasema.

Rais Kenyatta alikuwa ameahirisha ziara yake Ukambani kufuatia tofauti kati ya Bw Musyoka na magavana Kibwana, Alfred Mutua(Machakos), na Charity Ngilu (Kitui). Magavana hao walimlaumu Bw Musyoka kwa kuwa na nia ya kutumia ziara hiyo kujipigia debe kisiasa hasa azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, aliamua kuzuru baadhi ya miradi na kuepuka mikutano ya hadhara kutokana na kanuni za kuzuia msambao wa corona.

Jana, aliandamana na magavana hao na viongozi wengine akiwemo kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kukagua ujenzi wa bwawa kubwa la Thwake, kaunti ya Makueni.

Akihutubia viongozi wa Ukambani Rais Kenyatta alikariri umuhimu wa muundomsingi bora katika maendeleo akisema miradi inayoendelea ya barabara, maji na stima itasaidia kuimarisha uchumi wa Kenya.

Rais alisema kwamba kunapokuwa na muundomsingi bora, Wakenya wataweza kuendesha biashara zao, kuchuma utajiri na kubuni nafasi za ajira kwa vijana wa nchi hii.

Alishangaa kwa nini baadhi ya Wakenya wanapinga ongezeko la uwekezaji wa serikali katika miradi ya muundomsingi akisema wasiwasi wao hauna msingi.

You can share this post!

Mamia wapoteza kazi UoN huku idara zikivunjwa

Mkenya aliyechapwa viboko na Mchina kulipwa Sh3 milioni