Kalonzo kuamua leo ikiwa ama atawania au atarejea Azimio

Kalonzo kuamua leo ikiwa ama atawania au atarejea Azimio

JUSTUS OCHIENG NA MOSES NYAMORI

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka leo Jumatatu ataamua ikiwa atawania urais kivyake au atarejea katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na kumuunga mkono Raila Odinga.

Bw Musyoka anatarajiwa kutoa tangazo hilo atakapokuwa na jumla ya wawaniaji 500 wa viti mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho.

Mkutano ambao utafanyika katika mkahawa wa Stoni Athi Resort, Kaunti ya Machakos, unafanyika siku ya mwisho ambayo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inahitaji wawaniaji urais kuwasilisha sahihi za wafuasi wao kutoka angalau kaunti 24 wanaounga mkono azma zao.

Wawaniaji urais pia wanapaswa kuwasilisha nakala za vitambulisho vya kitaifa au paspoti za watu hao 2,000 kutoka kila moja ya kaunti hizo, ambao sharti wawe wamesajiliwa kuwa wapigakura.

Jana Jumapili, wandani wa Bw Musyoka hawakutaka kubaini waziwazi ikiwa kiongozi huyo wa Wiper ametimiza matakwa hayo, na mengine yaliyowekwa na IEBC.

Hata hivyo, walithibitisha kuwa Bw Musyoka atakutana na wawaniaji wa chama hicho kujadili masuala yanayohusiana na uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Naibu mwenyekiti wa Wiper, Bw Mutula Kilonzo Junior, alisema kuwa ingawa mkutano wa leo Jumatatu uliitishwa kupanga mikakati itakayowawezesha wawaniaji hao kushinda, masuala ya Azimio pia yataangaziwa.

“Hatujawahi kukutana tangu tulipokamilisha kura za mchujo. Twapaswa kupanga mikakati na kujadili mbinu za kushinda katika uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo, masuala ya Azimio pia yatachipuza,” Bw Kilonzo akaambia Taifa Leo.

  • Tags

You can share this post!

Karua afufua Raila katika Mlima Kenya

TAHARIRI: Afya ya uzazi kuhusu fistula itengewe pesa na...

T L