Habari Mseto

Kalonzo kuipigia debe BBI

September 13th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka ametangaza Jumapili kuwa atazunguka kote nchini kuupigia debe mpango wa maridhiano (BBI) akisema ni wenye manufaa kwa taifa.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari baada ya kutamatika kwa mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) wa chama hicho katika mkahawa wa Maanzoni Lodge, Kaunti ya Machakos, Musyoka amesema baraza hilo ndilo lilipitisha uamuzi huo.

“BBI inaandaa jukwaa kwa mdahalo wa kitaifa kuhusu njia za kuliboresha taifa hili wala sio mashindano ya watu binafsi,” akasema.

Akaongeza: “BBI inatoa nafasi kwetu kuimarisha ugatuzi na nafasi ya kuboresha Katiba ya sasa. Muhimu zaidi ni kwamba inatoa nafasi ya kipekee ya kutimiza matakwa ya mamilioni ya Wakenya ambao wanahisi kutengwa katika mfumo wa uongozi ulioko sasa.”

Hata hivyo, Bw Musyoka alibaini kuwa chama cha Wiper hakiungi mkono pendekezo la kuanzishwa kwa serikali za majimbo.

Suala hilo limekuwa likipigiwa debe na kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye ni mkereketwa sugu wa mpango wa BBI.

“Ni wazi kuwa Wakenya hawako tayari kwa mfumo wa utawala wa majimbo. Kwa mtazamo wetu kama Wiper kile ambacho ni muhimu ni kuimarisha ugatuzi ili uwafaidi wananchi wa kawaida. Njia moja ya kufikia hili ni kubuniwa kwa Hazina ya Ustawi wa Wadi (WDF),” akaeleza Bw Musyoka ambaye ni Makamu wa Rais wa zamani aliyehudumu katika muhula wa pili wa utawala wa Rais wa zamani Mwai Kibaki.

Pendekezo la kufanya wadi kuwa kitovu cha maendeleo lilitolewa kwa mara ya kwanza na kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Ekuru Aukot kupitia mpango wake wa mageuzi ya Katiba uliojulikana kama ‘Punguza Mzigo Punda Amechoka’.

Mchakato wa BBI ulianzishwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kupitia muafaka kati yao mnamo Machi 9, 2018, maarufu kama Handisheki.

Maridhiano hayo ya kisiasa yalikomesha ghasia ambazo zililipuka nchini kufuatia uchaguzi mkuu wa 2017 baada ya matokeo ya urais kusababisha ubishi.

Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo hayo na uchaguzi mwingine wa urais ukaitishwa na kufanyika mnamo Oktoba 28, 2017, na ukasusiwa na Bw Odinga.

Wakati huo huo, licha ya kwamba chama cha Wiper kilitia saini mkataba wa ushirikiano na chama tawala cha Jubilee, Bw Kalonzo alisema chama chake kimeanzisha mpango wa kujiimarisha kwa lengo la kudhamini mgombeaji urais 2022.

“Hatua ya mwanzo katika mpango huu ni kuanzisha shughuli ya usajili wa wanachama wapya. Shughuli hiyo itaendeshwa kwa njia ya dijitali hivi karibuni,” kiongozi huyo wa Wiper akaeleza.