Kalonzo, Muthama, Mutua kupimana ubabe kampeni zikianza kwa kishindo

Kalonzo, Muthama, Mutua kupimana ubabe kampeni zikianza kwa kishindo

Na BENSON MATHEKA

KAMPENI za uchaguzi mdogo wa kiti cha useneta Kaunti ya Machakos zilianza kwa kishindo baada ya wagombeaji wanane kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kauli za viongozi mbali mbali walioandama na wagombeaji hao zilionyesha uchaguzi huo utakuwa wa kupima ubabe kati ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa kaunti hiyo Alfred Mutua na aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo na mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama.

Kiti hicho kilibaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Bw Bonface Kabaka. IEBC imetangaza kwamba uchaguzi mkuu utafanyika Machi 18  mwaka huu.

Kuanzia Jumanne wagombeaji wa vyama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, Maendeleo Chap Chap cha Gavana  Mutua naWiper cha aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka wamekuwa piga kambi mjini Machakos.

Bw Mutua anawarai wakazi kumpigia kura mgombeaji wa chama chake Bw Mutua Katuku akisema ni mwanasiasa mkomavu na mwenye uzoefu. Bw Katuku ni mbunge wa zamani wa eneo la Mwala na alihudumu kama waziri wa maji.

“Nipatieni seneta aliye na uzoefu wa miaka mingi anisaidie kufanya maendeleo haraka badala ya kunisumbua,” Dkt Mutua aliwaambia wakazi baada ya Bw Katuku kuidhinishwa na IEBC.

Aliwapuuza wapinzani wanaosema ni makosa kwa gavana na seneta kutoka chama kimoja.

 “Kuna kaunti nyingi ambazo gavana na seneta wanatoka chama kimoja kwa hivyo msipotoshwe na porojo,” alisema.

Aliyekuwa seneta wa Kaunti hiyo Johnson Muthama aliongoza wanachama wa kundi la ‘Tangatanga’ kumpigia debe mgombeaji wa UDA, Urbanus Muthama Ngengele.

Bw Ngengele ambaye aliidhinishwa na IEBC Jumatatu, aliungana na wanachama wa ‘Tangatanga’ wakiwemo Kimani Ichungwah, Kipchumba Murkomen, Hassan Omar, Victor Munyaka, Aaron Cheruiyot na Rigathi Gachagua kuwalaumu Bw Musyoka na Dkt Mutua kwa kupuuza jamii ya Wakamba.

Viongozi hao walisema kuchagua mgombeaji wa chama cha Wiper, Agnes Kavindu Muthama ni kurudisha nyuma Kaunti ya Machakos.

“Uchaguzi huu sio wa Machakos pekee, ni uchaguzi kuhusu hatima ya Kenya. Tupatieni Seneta wa kwanza wa chama cha UDA,” alisema Bw Cheruiyot.

“Lengo letu ni kuunda serikali baada ya 2022 na tunataka kuanza na Machakos,” alisema Bw Muthama.

Viongozi wa ‘Tangatanga’ walidai kwamba kupigia kura mgombeaji wa Maendeleo Chap Chap au wa Wiper ni kuchagua BBI ambayo walidai haina cha kuwafaidi Wakenya masikini.

Naye Bw Musyoka aliungana na viongozi wa vyama vya kisiasa wanaounga BBI, Musalia Mudavadi (Amani National Congress) Moses Wetangula (Ford Kenya) na Gideon Moi ( Kanu)  kumpigia debe Bi Kavindu akisema ndiye anayeelewa shida za wakazi wa Kaunti ya Machakos.

Alisema kwamba ushindi wa Wiper katika uchaguzi huo utaimarisha nafasi ya kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bi Muthama aliwakosoa wanaodai kwamba hana uzoefu na ujasiri wa kuwa kiongozi akisema amekuwa katika nyadhifa nyingi za uongozi.

Aliwataka wapinzani wake kutoingiza masuala ya ndoa yake na Muthama katika siasa akisema kwamba anamheshimu kama baba ya watoto wake.

“Sijawahi kumdharau Bw Muthama au kumzungumzia hadharani, naye pia anafaa kunipa heshima yangu,” alisema.

You can share this post!

Serikali yaweka mikakati ya kuwakabili wauzaji na watumiaji...

Chipu kutetea Kombe la Afrika mwezi Machi, ratiba ya...