Habari MsetoSiasa

Kalonzo naye afika kwa Mzee Moi kusaka baraka

November 16th, 2018 2 min read

FRANCIS MUREITHI na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka Ijumaa alimtembelea Rais mstaafu Daniel Moi nyumbani kwake Kabarak, Nakuru kusaka baraka anapoanza kibarua kama mjumbe wa amani nchini Sudan Kusini.

Kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook, Bw Musyoka alithibitisha kupokea baraka hizo wakati wa ziara hiyo ambapo alioandama na viongozi chipukizi kutoka ngome yake ya Ukambani.

“Mzee Moi alinipa baraka nikiungana na viongozi wengine nikiendeleza harakati za kupalilia amani nchini, katika ukanda huu na kote duniani. Vile vie ni fahari yangu kwamba tulijadili masuala ya humu nchini, tukashiriki chakula na kuomba pamoja,” akasema.

Ziara ya Kalonzo inajiri wiki moja baada ya mazishi ya babake, marehemu Peter Musyoka Mairu, ambapo Mzee Moi alituma risala zake kupitia mwanawe, Seneta Gideon Moi.

Kiongozi huyo wa Wiper aliandama na maseneta; Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Enock Wambua (Kitui) na mwanawe, Kennedy Musyoka ambaye ni mbunge wa Afrika Mashariki.

Katika hotuba yake, Moi aliwashauri viongozi wenye umri mdogo kuzingatia uadilifu wanapohudumia wananchi.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa wanahabari na msemaji wake, Lee Njiru, Rais huyo mstaafu alisema viongozi wenye umri wa chini wanapaswa kutoa ulinzi maalum kwa wanajamii wa jinsia zote, haswa wale waliopungukiwa kimasomo.

“Watu wasioelimika, haswa wale wanaoishi katika maeneo ya mashambani, wanahitaji kupewa mwelekeo mwema na viongozi kama hao,” akasema Mzee Moi.

Alikariri haja ya viongozi vijana kupalilia umoja wakati huu ambapo jamii inakabiliwa na changamoto nyingi.

“Viongozi vijana hawafai kuhudumia watu waliosoma pekee bali hata wale ambao hawakupevuka kimasomo,” Mzee Moi akasema kwenye taarifa.

Alisema bila umoja, itakuwa vigumu kwa viongozi vijana kuafikia maendeleo huku akiwahimiza kufanya kazi kwa bidii”.

“Nilipoteuliwa Mbunge wa Rift Valley 1955 nilihudumia eneo hilo lote. Nilikuwa nikisafiri kwa gari aina ya Landrover,” Mzee akafichua.

Aliwakumbusha viongozi walioandamana na Bw Kalonzo kuwa, kwa sasa eneo hilo lina zaidi ya wabunge 40 na hivyo itarajiwa utoaji huduma kuimarika hata zaidi.

Mzee Moi alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa afya nzuri ambayo imemwezesha kuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu.

Alisema afya nzuri ndio imemwezesha kupata nguvu na bidii ya kuimarisha maslahi ya Wakenya bila kujali miegemeo yao kisiasa na kijamii.

Wakati huo huo, Moi alikutana na wabunge; Silas Tiren (Moiben), Elijah Memusi (Kajiado ya Kati) na William Kamket (Tiaty).