HabariSiasa

KALONZO NJIA PANDA: Nijiunge na Ruto au Raila?

July 18th, 2018 2 min read

Na WYCLIFFE MUIA

KINARA wa Wiper, Kalonzo Musyoka anakabiliwa na shinikizo za kuamua iwapo atii viongozi wenzake Ukambani wanaomsukuma ashirikiane na Naibu Rais William Ruto katika maandalizi ya uchaguzi wa 2022, au akwame na Raila Odinga.

Duru zinadokeza kwamba viongozi wengi Ukambani wameanza kumwondokea Bw Odinga kutokana na kile wanachosema ni “usaliti” aliofanyia jamii hiyo alipoamua kivyake kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta bila kushauriana na Bw Musyoka.

Pia wanahisi kusalitiwa na chama cha Bw Odinga cha ODM kuhusiana na uchaguzi wa 2022, ambapo walipobuni Muungano wa NASA kulikuwa na makubaliano watasimama nyuma ya Bw Kalonzo. Lakini wakuu wa ODM wamekuwa wakisema watakuwa na mgombeaji wao, na juhudi za kumtaka Bw Odinga kutangaza msimamo wake kuhusu suala hilo hazijazaa matunda kwani hajatamka lolote kulihusu.

Mnamo Jumatatu, Seneta wa Kituo Enock Wambua aliongoza wabunge wa Kitui katika mkutano na Bw Ruto nyumbani kwake Karen, Nairobi.

Bw Wambua alisema japo kikao hicho hakikuwa cha kisiasa, chama cha Wiper kiko tayari kushirikiana na Bw Ruto. “Mkutano wetu na Naibu Rais uliangazia tu masuala ya maendeleo katika eneo letu. Masuala mengine ya siasa sitayazungumza mimi, kuna msemaji wetu ambaye atatoa taarifa baadaye,” alisema Bw Wambua.

Bw Musyoka amekuwa akikabiliwa na shinikizo kutoka uongozi wa chama chake cha Wiper, ambapo Mwenyekiti Prof Kivutha Kibwana amemwambia hadharani kusahau muafaka wake na Bw Odinga wa 2017, na kutafuta marafiki wengine wa kisiasa.

“Wiper pamoja na kinara wetu Kalonzo tunajuta kuunga mkono Raila kwa miaka kumi. Sasa wakati umefika kwa Kalonzo kujisimamia kisiasa na kusaka marafiki wapya wa siasa,” alisema Prof Kibwana baada ya Bw Odinga kusalimia na Rais Kenyatta.

Licha ya shinikizo hizo, Bw Musyoka anaonekana kumkwamilia Bw Odinga huku akisisitiza kuwa kiongozi wa ODM bado ndiye kiongozi wa upinzani nchini na muafaka kati yake na rais unapaswa kupewa nafasi ya kuunganisha taifa.

Wachanganuzi wanasema Bw Musyoka anafanya hivyo ili kuhakikisha amerithi ngome za kisiasa za Bw Odinga ifikiapo 2022.

Tayari Bw Musyoka ametangaza wazi kuwa katika kura za 2022 hatakuwa mgombeaji mwenza wa urais wa mtu yeyote liwe liwalo.

Wiki iliyopita Bw Musyoka alitoa kauli nzito mbele ya Bw Odinga kuwa amekuwa mkarimu kisiasa kwa kuunga wawaniaji wa urais zaidi ya mara tatu kisha baadaye wanamtema kama kiazi moto.

Katika kile kilionyesha kuwa viongozi wengi hasa katika Kaunti ya Kitui, anakotoka Bw Musyoka, ni Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu pekee aliyehudhuria hafla ya Bw Odinga wiki jana, huku baadhi ya wabunge waliosusia wakisema walifanya hivyo ili kupinga ‘usaliti’ wa kisiasa wa Bw Odinga dhidi ya jamii ya Wakamba.

Baadhi ya wandani wengine wa Bw Musyoka wanamtaka asalie ‘katikati’ na asipinge muafaka kati ya Raila-Uhuru na pia asipuuze ‘mwaliko’ wa Bw Ruto.

“Hatuna kinyongo na Raila lakini pia si makosa tukishirikiana na Ruto katika siasa za 2022,” alisema Prof Kibwana.

Magavana Ngilu, Kibwana, Spika wa Kaunti ya Kitui George Ndoto pamoja na mwaniaji wa ugavana wa Machakos Wavinya Ndeti walimtaka Bw Musyoka kuangazia urais 2022 kivyake bila kutegemea mwanasiasa yeyote.

Kuna wasiwasi kuwa iwapo Bw Musyoka ataendelea kushirikiana na Bw Odinga huenda baadhi ya wandani wake wakamhepa na kuunga mkono azma ya urais ya Bw Ruto.

Pia, iwapo Bw Musyoka atakubali kushirikiana na Bw Ruto, atakuwa na kibarua kigumu cha kumshawishi Bw Ruto kuzima ndoto yake ya kuwa na rais na kuendelea kuwa naibu rais.