Kalonzo sasa apanda bei

Kalonzo sasa apanda bei

Na LEONARD ONYANGO

USHAWISHI wa kisiasa wa kinara wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka unaonekana kuongezeka huku wadadisi wakisema kuwa ataamua mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Baada ya kinara wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Bw Moses Wetang’ula kuungana na Naibu wa Rais William Ruto chini ya muungano wa Kenya Kwanza, wadadisi wanasema kuwa Bw Musyoka ndiye sasa atakayeamua mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Seneta wa Makueni, Bw Mutula Kilonzo Junior amemfananisha Bw Musyoka sawa na jiwe lililotajwa katika Biblia ambalo lilikataliwa na wajenzi (waashi) lakini umuhimu wake ukabainika baadaye.

Kulingana na Bw Kilonzo Jr, mrengo ambao Bw Musyoka ataegemea utashinda urais katika uchaguzi mkuu ujao.

“Bw Musyoka sasa ni jiwe ambalo wajenzi walikataa. Sasa anatafutwa na wajenzi baada ya kugundua umuhimu wake katika siasa zinazohusu uchaguzi ujao,” akasema Bw Mutula Jr.

Bw Javas Bigambo, wakili na mtaalamu wa masuala ya utawala, anasema kuwa itabidi kinara wa ODM, Bw Raila Odinga au Dkt Ruto watumie mbinu zote kumnasa Bw Musyoka.

“Bila shaka Bw Musyoka anashikilia ufunguo wa Ikulu kwa sababu anadhibiti asilimia kubwa ya kura milioni mbili za eneo la Ukambani. Bw Odinga au Dkt Ruto wanafaa kunyenyekea kwa Kalonzo ili wamnase. Atakayefanikiwa kuvutia Kalonzo upande wake atakuwa na nafasi kubwa ya kushinda urais Agosti 9,” anasema Bw Bigambo.

Jana Alhamisi, Bw Musyoka aliongoza vinara wenzake wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA); Mabw Gideon Moi (Kanu) na Cyrus Jirongo (United Democratic Party) kujipigia debe katika Kaunti ya Kitui.

Viongozi hao wa OKA leo watazuru Kaunti ya Makueni kabla ya kuelekea Kaunti ya Machakos kesho.

Wadadisi wanasema kuwa Kalonzo analenga kutumia ziara hiyo katika kaunti za Ukambani kupunguza ushawishi wa Bw Odinga na Dkt Ruto ambaye amekuwa akizuru eneo hilo mara kwa mara.

Baadhi ya viongozi wa Ukambani wanaounga mkono Naibu wa Rais ni aliyekuwa seneta wa Machakos Jonhson Muthama, naibu gavana wa zamani wa Nairobi Jonathan Mueke, naibu gavana wa Makueni Adelina Mwau na wabunge Vincent Munyaka (Machakos Mjini), Nimrod Mbai (Kitui Mashariki) na Vincent Musyoka (Mwala).

Naye Bw Odinga anaungwa na magavana wote watatu wa kaunti za Ukambani; Bi Charity Ngilu (Kitui), Prof Kivutha Kibwana (Makueni) na Dkt Alfred Mutua wa Machakos. Bi Ngilu na Prof Kibwana wamekuwa katika mstari wa mbele kumshinikiza Bw Musyoka kuunga mkono Bw Odinga anayepeperusha bendera ya muungano wa Azimio la Umoja.

“Kalonzo ajiunge na Azimio la Umoja tuunde serikali aache kuzunguka katika kaunti za Ukambani huku akidai kwamba anataka kuwa rais wa Kenya,” akasema Bi Ngilu.

Gavana wa Makueni ameshikilia kuwa atasaidia Bw Odinga kupata asilimia 97 ya kura katika kaunti yake hata bila kuungwa mkono na Kalonzo.

“Nasikia Stevo (Kalonzo) atakuja Makueni Ijumaa (leo); ingekuwa vyema aje na ujumbe wa Azimio la Umoja. Lakini akidai kwamba atawania urais kupitia muungano wa OKA anapoteza wakati,” akaonya Prof Kibwana.

Bw Bigambo, hata hivyo, anaonya kuwa Bw Musyoka huenda akakosa ushawishi wa kisiasa eneo la Ukambani iwapo ataamua kuwania urais.

“Ni kweli kwamba Kalonzo ana ushawishi mkubwa katika eneo la Ukambani kwa sasa. Lakini akifanya makosa ya kuwania urais, wapigakura wa eneo hilo huenda wasimpigie kwa sababu wanajua hataenda popote,” anasema Bw Bigambo.

Viongozi wa ODM waliohojiwa na Taifa Leo na wakaomba majina yao yabanwe kwa kuhofia kusutwa na wakuu wao, walisema wameelekeza matumaini yao kwa Rais Kenyatta kutumia ukuruba wake na kinara wa Wiper kumshawishi kuunga mkono Bw Odinga.

Wanahofia kuwa huenda Bw Odinga akawa na kibarua kigumu kushinda urais Agosti 9 iwapo Bw Musyoka atajiunga na Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

WIKI YA LUGHA ZA KIAFRIKA: Mikakati ya kukuza matumizi ya...

TAHARIRI: Kiswahili kimeathiriwa pakubwa na sera baguzi

T L