Habari Mseto

KALRO: Wadudu hatari wamevamia Afrika

May 26th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Huku mamia ya wakulima wa mahindi wakizidi kukabiliana na viwavi hatari, shirika la utafiti wa kilimo na mifugo (KALRO) limeonya kuhusu aina mpya ya wadudu waharibifu.

Wadudu hao tayari wameingia Afrika na wanaharibu mimea ambayo ina uwezo wa kustahimili wadudu na upungufu wa mvua.

Mimea hiyo ni kama mhogo, viazi na mchicha. Huenda hali hiyo ikasababisha upungufu zaidi wa chakula nchini.

Hivi sasa, wadudu hao wanaendelea kutatiza wakulima Benin, Cameroon, Gabon na Nigeria, na huenda wakafika nchini, alionya afisa wa KARLO Jumatano.

Huenda wadudu hao wakasababisha hasara zaidi wakati ambapo viwavi hatari vimewafanya wakulima kupata hasara ya Sh3.5 bilioni.