Kamagiras 20 wakamatwa na polisi katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Reuben

Kamagiras 20 wakamatwa na polisi katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Reuben

NA SAMMY KIMATU

skimatu@ke.nationmedia.com

KINARA wa polisi eneo la Makadara Bw Timon Odingo na mkuu kitengo cha DCIO, Bw Felix Nyamai walishirikiana kuvunja mipango ya kundi haramu la wahalifu wanaojiita Kamagiras.

Katika operesheni hiyo iliyofanyika maeneo ya mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Reuben, washukiwa 20 walikamatwa.

Isitoshe, polisi walinasa pikipiki nne zinazoaminika kuwa ziliibiwa.

Waendeshaji bodaboda zilizonaswa waliziacha na kutoroka baada ya kugundua polisi walikuwa wakiendesha operesheni.

Bw Odingo aliambia Taifa Leo kwamba washukiwa hufanya shughuli ya kulazimisha kila matatu kulipa Sh100 kabla ya kubeba abiria katika steji.

Zaidi ya hayo ni kwamba washukiwa huwa katika steji za matatu katika barabara mbalimbali katika Eneo la Viwanda, barabara ya Jogoo na Mombasa Road miongoni mwa zingine.

“Waendeshaji walitoroka walipogundua kuwa polisi waliovalia kiraia walikuwa wakifanya operesheni katika mtaa wa Reuben. Genge hilo hutoza kila matatu Sh100 kama ada ya kubeba wasafiri kwenye steji la matatu. Matatu isipotoa pesa, mlango wa matatu hufungwa kwa nguvu ili abiria asiingie kisha dereva hulazimizwa kuondoa gari lake,” Bw Odingo alisema.

Naye mkuu wa kitengo cha uhalifu wa jinai, Bw Nyamai aliongeza kuwa wanawazuilia washukiwa hao kwa uchunguzi zaidi jambo ambalo wanaamini litapelekea kukamatwa kwa viongozi wao kwa vile ‘wanamgambo’ ni genge lililopangwa.

Polisi walisema sekta ya matatu inapoteza mamilioni ya pesa kutokana na genge hilo.

“Katika paradiso ya genge, viongozi huendesha Prado na magari mengine ya bei ghali lakini ukienda kwenye steji za matatu, utakuta vijana ‘wasio na matumaini’.

Alitoa wito kwa wananchi kupata uhamasishaji na taarifa za kujitolea kwa vyombo vya usalama.

“Ninawaomba wananchi kuwapa polisi habari zinazoweza kupelekea kukamatwa kwa wahalifu kama hao miongoni mwa jamii ili watu waishi kwa amani,” Bw Odingo anaongeza.

Changamoto kubwa katika idara ya polisi, Bw Odingo anasema ni wahalifu kwa kawaida kubadilisha mbinu mara kwa mara.

Taarifa za polisi zilieleza kuwa awali, genge hilo lilikuwa likitambulika kirahisi kwa kuwa na rasta (dreadlock).

Baadaye walibadilika na kutumia kitambaa cha kichwa cha Wakorino, wakabadilika na kuanza kunusa tumbaku hadharani ila siku hizi wanafanana na Mkenya mwingine yeyote wa kawaida.

“Ni vigumu kuwakamata kwa kuwa hawana alama yoyote. Hata mkiwakamata wale hitisha pesa kwa magari katika steji na kuwapeleka mahakamani ni kazi ya bure. Wanapewa bodi na hata bodi iwe kubwa kiasi gani, ‘wakubwa’ wao hulipa bodi hizo papo hapo,” polisi wasema.

  • Tags

You can share this post!

Chumvi nyingi huzidisha msongo wa mawazo – Utafiti

BORESHA AFYA: Kwa afya ya akili

T L