KimataifaUncategorized

Kamala Harris alimtokea Tim Walz kimwizimwizi ‘kama Yesu siku za mwisho’


NUSRA Timothy Walz akose uteuzi wake kama mgombeaji mwenza wa Kamala Harris alipokosa kushika simu yake ya kumfahamisha kuwa ndiye chaguo bora miongoni mwa Democrats.

Ni hali inayosawiri simulizi ya Biblia ambayo inamnukuu Yesu Kristu akisema atakuja kama mwizi,  ambayo inafasiriwa kuwa wengi hawatajua ujio wake huo.

Mgombeaji wa urais wa Chama cha Democratic, Kamala Harris amefichua namna Gavana wa Minnesota, Walz alivyokosa kushika simu yake aliyompigia kumpa habari kwamba amemteua kuwa mgombeaji-mwenza katika uchaguzi wa urais wa Novemba 5, mwaka huu.

Wakiwa kwenye mazungumzo ya moja kwa moja, Harris alimuuliza Tim kwa nini hakushika simu yake alipompigia.

“Nilikupigia simu Tim. Hukushika simu yangu. Shida ilikuwa gani,” Harris alimuuliza Tim huku akicheka kwa nguvu.

Naye Tim alijitetea akisema, “Nilipigiwa simu muhimu sana maishani ila sikushika kwa kuwa sikujua aliyekuwa anapiga.”

Tim alisema kuwa anafurahia sana kuwa mgombeaji-mwenza wa Harris.

“Nafurahia sana kuteuliwa katika nafasi hii. Ni nafasi nadra sana.”

“Tutashirikiana hadi mwisho. Tutashinda pamoja,” Harris akamhakikishia Tim.

Walz, 60, ambaye ni shujaa wa zamani wa Jeshi la Kitaifa la Amerika na mwalimu, alichaguliwa kama Mbunge katika Bunge la Wawakilishi mnamo 2006 ambako alihudumu kwa miaka 12 kabla ya kuchaguliwa Gavana wa Jimbo la Minnesota mnamo 2018.

Akihudumu kama Gavana, Walz alitetea ajenda endelevu zilizojumuisha utoaji wa lishe shule bila kulipiwa, malengo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, punguzo la ushuru kwa watu wa tabaka la kati na kuanzishwa kwa sera za wafanyakazi kulipwa wakiwa likizoni katika jimbo la Minnesota.

Walz anaonekana na wengi kama mwenye ujuzi wa kuwavutia wapiga kura Weupe na wa maeneo ya mashambani ambao katika miaka michache iliyopita wamemuunga mkono mgombeaji wa chama cha Republican, Donald Trump. JD Vance ndiye mgombeaji-mwenza wa Trump.

Harris alimteua Walz badala ya Gavana wa Pennsylvania Josh Shapiro, ambaye alitarajiwa kumpa ushindi katika jimbo hilo muhimu.