Habari

Kamanda motoni kupuuza Ruto

November 30th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU na NICHOLAS KOMU

KIZAAZAA kilizuka Ijumaa katika hafla ya harambee KATIKA kaunti ya Kirinyaga baada ya Mbunge Maalum Maina Kamanda kuzomewa vikali kwa kutomtaja Naibu Rais William Ruto kuwa miongoni mwa viongozi waliochangia katika ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Bw Kamanda alikuwa akiwahutubia wakazi kwenye hafla ya kuchangisha pesa iliyoandaliwa na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho katika Shule ya Upili ya Gathuthu-ini, eneobunge la Ndia alipokosa kumtaja Dkt Ruto.

Hafla hiyo pia ilikuwa imehudhuriwa na waziri katika wizara hiyo Dkt Fred Matiang’i.

Kwenye hotuba yake, Bw Kamanda alikosa kumtambua Dkt Ruto kama mshirika mkuu wa Rais Kenyatta katika Serikali ya Kitaifa.

Mbunge huyo, ambaye ni mwanachama wa kundi la ‘Kieleweke’ aliwataja Rais Kenyatta na Bw Odinga mara kadhaa kama viongozi ambao “wameleta amani nchini na uthabiti wa kisiasa” bila kumtaja Dkt Ruto, hali iliyowakasirisha wakazi.

“Itakapofika 2022, kwa maoni yangu, atakayekuwa rais…” akasema Bw Kamanda kabla ya kukatizwa na wakazi.

Wakiwa na hasira, wakazi walianza kumzomea wakiimba “Ruto, Ruto,” hadi akalazimika kukatiza hotuba yake.

Alipozidiwa, alimkabidhi Mwakilishi wa Wanawake kaunti ya Kirinyaga, Bi Wangui Ngirichi ambaye ni mshirika wa Dkt Ruto kipaaza sauti ambaye alifaulu kuwatuliza wakazi.

Hali hiyo pia ilimlazimu mwenyeji wa hafla hiyo, Dkt Kibicho, kuingilia kati ili kutuliza taharuki iliyokuwa ikitanda.

Kwa hasira,Dkt Kibicho aliwaambia wale ambao hawakuridhishwa na hafla hiyo ama yaliyokuwa yakiendelea kuondoka mara moja.

Alisikitika kwamba viongozi wa kisiasa aliowaalika waligeuza hafla hiyo kuwa jukwaa la kisiasa.

“Ninasikitika kuwa baadhi ya viongozi niliowaalika wameegemea masuala ya kisiasa,”akasema.

Mawaziri wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Bw Joe Mucheru (Habari, Mawasiliao na Teknolojia), James Macharia (Uchukuzi), Keriako Tobiko (Mazingira), Peter Munya (Biashara na Viwanda) na George Magoha (Elimu).

Magavana waliokuwepo ni Anne Waiguru (Kirinyaga), Francis Kimemia (Nyandarua), Hasaan Joho (Mombasa), Joseph Ole Lenku (Kajiado), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), John Nyagarama (Nyamira) na Mutahi Kahiga (Nyeri).

Wengine

Viongozi wengine waliokuwepo ni Gladys Wanga (Homa Bay), Gathoni Wamucomba (Kiambu) kati ya wengine.

Kwenye hotuba yake, Dkt Matiang’i aliwakosoa vikali viongozi ambao wamekuwa wakimlaumu Dkt Kibicho kwa kuwa hasimu wa Dkt Ruto, akisema wanapaswa kumlaumu yeye binafsi na Rais Kenyatta.

“Ninachukua lawama zote kwa utendakazi wote wa vikosi vya usalama. Msiwahi kumlaumu katibu wangu (Kibicho) kwa matatizo ya kisiasa yaliyo ndani ama nje ya serikali. Kenya ina Rais mmoja (Kenyatta) ambaye huwa tunapokea maagizo kutoka kwake. Hatua zozote zinazochukuliwa na vikosi hivyo huwa agizo la Rais,” alisema Dkt Matiang’i.

Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kiambu Bi Gathoni Wamuchomba alisema kwamba, kuwa baadhi ya wabunge ni wafisadi na hawawezi kuaminiwa kuendesha mchakato wa utekelezaji wa ripoti ya BBI.

Kundi la ‘Tanga Tanga linalomuunga Dkt Ruto limekuwa likimlaumu Dkt Kibicho kwa kumdharau wazi Dkt Ruto.