Habari Mseto

KAMARI: Wafanyabiashara 17 wa kigeni wafurushwa

May 21st, 2019 1 min read

KENNEDY KIMANTHI na CHARLES WASONGA

JUMLA ya raia wa kigeni 17 wanaojishughulisha na biashara ya kamari kinyume chama sheria nchini Jumanne walifurushwa kutoka nchini katika juhudi za serikali za kudhibiti biashara hiyo nchini.

Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i kumwamuru Katibu wa Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa kuchunguza upya leseni za kazi za wageni ambao walituma maombi ya kupata kibali ya kufanya biashara zingine lakini wakaishia kuwekeza katika sekta ya Kamari.

Wale waliorejeshwa katika mataifa yao ni pamoja na raia wa China, Uturuki na Uhispania.

Wakati huu Kenya ina zaidi ya kampuni 30 za kamari na casino zilizosajiliwa, ingawa ni chache zinafanya kazi.

Mnamo Jumatatu, Waziri Matiang’i aliamuru Bw Kihalangwa kuchunguza upya leseni za kazi za wageni wote waliotuma maombi ya kuendesha biashara nchini.

“Hatuwezi kufumbia macho uozo katika sekta hii eti kwa sababu ni chanzo cha mapato… Zaidi ya asilimia 90 ya washirika katika biashara ya Kamari ni wageni. Wao hupelekea kiasi kikubwa cha pesa nchini mwao.

“Wimbi la kamari nchini umeleta madhara ya kijamii na kiuchumi huku likifaidi watu wachache matajiri, wengi wao ambao sio Wakenya na wanaishi nje ya nchi,” Dkt Matiang’i akasema wakati wa wadau katika sekta ya kamati katika Taasisi ya Mafunzo ya Utawala, Kabete, Nairobi.