Habari

Kamari: Wengi kuumia

July 13th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Serikali ya kunyima kampuni kubwa za kamari nchini leseni itaathiri pakubwa uchumi wa nchi.

Kwa kupokonywa leseni za kuhudumu, kampuni hizo zitalazimika kusitisha miradi ya mamilioni ya pesa ambayo zimekuwa zikifadhili.

Kulingana na kampuni hizo, kufikia jana serikali haikuwa imefafanua sababu za kuzipokonya leseni licha ya kutimiza mahitaji yote ya kisheria.

Kwenye taarifa, kampuni ya Betin ambayo ina mtandao wa maduka yanayoajiri maelfu ya vijana nchini ilisema, hatua ya serikali italemaza uchumi na ukuaji wa vipawa nchini.

“Serikali haijafafanua sababu za kusema hatujatimiza mahitaji ya kisheria. Tangu tulipoanza shughuli zetu, tumekuwa tukilipa ushuru chini ya sheria ya kamari,” Betin ilisema.

Kampuni hiyo imekuwa ikifadhili timu ya soka ya taifa ya Harambee Stars, hasa ilipokuwa ikijiandaa kwa mechi za kombe bingwa barani Afrika (AFCON).

Mapema mwaka 2019 kampuni hiyo ilitumia Sh20 milioni kusaidia timu hiyo na ilikuwa na mipango ya kuendelea kuifadhili.

Kampuni hiyo pia imekuwa ikisaidia klabu ya soka ya Sofapaka ambayo imekuwa ikikuza vipawa vya wanasoka chipukizi. Mnamo 2017 na 2018, Betin ilitumia zaidi ya Sh50 milioni kufadhili miradi ya soka nchini.

Katika maduka yake kote nchini, kampuni hiyo imeajiri zaidi ya vijana 2,500 moja kwa moja na ina zaidi ya wafanyakazi 200 katika afisi yake.

Kwa mwezi, wamiliki wa maduka hayo walikuwa wakipata Sh120,000.

Aidha, imekuwa ikitoa matangazo ya mamilioni ya pesa kwa kampuni za humu nchini na kuchangia kuajiri maelfu ya vijana.

Serikali haikuisaza iliposimamisha leseni za kampuni 27 za kamari nchini ikisema hazijatimiza mahitaji yote ya kisheria.

Miongoni mwa masharti hayo ni kulipa ushuru, kutoshirikisha watu walio na umri wa chini ya miaka 18, kuhusisha watu maarufu kama wasanii kwenye matangazo ya kibiashara na kutoa onyo kwenye matangazo hayo kuhusu athari za uraibu wa kamari.

Mnamo Jumatano, BCLB iliagiza kampuni za Safaricom, Telkom na Airtel kufunga nambari zote za malipo na arafa za kampuni zilizopokonywa leseni.

Kulingana na kampuni hizo, serikali ilichukua hatua hiyo kwa nia mbaya na itaathiri uchumi wa nchi.

Yasikitika

Kwenye taarifa Ijumaa, kampuni ya SportPesa ilisema ilisikitishwa na hatua ya BCLB ya kufunga nambari zake licha ya kuwa mahakama iliagiza serikali kutoichukulia hatua.

Kampuni hiyo ilidai kwamba, imekuwa ikilipa kodi na kutimiza mahitaji yote ya kisheria nchini mbali na kuchangia maendeleo katika sekta tofauti.

“Biashara yetu imeinua kwa kiwango cha kipekee michezo na maendeleo nchini na hatujasita kuwekeza katika miradi ya jamii,” ilieleza taarifa ya Sportpesa muda mfupi baada ya nambari zake za Paybill na arafa kuzimwa.

“Hii imeshuhudiwa katika mchango wetu katika sekta kama kandanda, ndondi, raga na miradi ya kijamii kama maji, mazingira na kuimarisha vipawa nchini,” ilisema Sportpesa.

Kampuni hiyo ilisema itaelekea mahakamani kupinga hatua ya serikali.

“Tunataka kuhakikishia wateja wetu na wadau kwamba, tutapinga vitendo hivi na tutaendelea kuwasiliana na wadau wakuu kwa lengo la kutatua mzozo huu haraka iwezekanavyo,” alisema.

Mwanzoni mwa mwaka 2019 serikali ilisema uchezaji kamari umekuwa hatari kwa usalama wa taifa na kutoa masharti makali kabla ya kupata upya leseni za kuhudumu nchini.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alisisitiza kuwa nusu ya kampuni hizo hazingeruhusiwa kuhudumu nchini kuanzia Julai.

Mnamo Jumatano, Serikali iliagiza kampuni za mawasiliano ya simu na Mamlaka ya Mawasiliano (CA) kufunga nambari ambazo kampuni hizo zilikuwa zikitumia kwa mchezo huo.

Kampuni zilizoathiriwa ni SportPesa, Betin, Betway. Betpawa, Premierbet, Lucky 2 U, 1XBet, Mozzartbet, Dafabet, World Sport Bet, Atari Gaming, Palmsbet na Bet Boss.

Nyingine zilizopokonywa leseni ni Betyetu, Elitebet, Bungabet, Cysabet, Nestbet, Easybet, Kick Off, Millionaire Sports Bet, Kenya Sports Bet na Eastleighbet.