Kamatakamata ya wasiovalia maski yafika mitaani

Kamatakamata ya wasiovalia maski yafika mitaani

Na SAMMY WAWERU

MAAFISA wa polisi wamefanya msako mkali Jumatano katika eneo la Zimmerman, kiungani mwa jiji la Nairobi kutia nguvuni wasiovalia maski.

Kamatakamata hiyo ilianza asubuhi, maafisa wa polisi kutoka kituo cha Kasarani wakipiga doria kwa lori na gari dogo.

Wakazi kadha walijipata kuandamwa na mkono wa sheria, kwa kupuuza kuvalia kifaa hicho muhimu.

“Tunashangaa ikiwa ni lazima watu washurutishwe kulinda maisha yao kwa kuvalia barakoa. Tutaendelea kuchukulia hatua wanaopuuza sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti maenezi ya virusi vya corona,” akaonya mmoja wa maafisa waliopiga doria.

Kwa muda wa wiki kadha zilizopita, Shirika la Kuimarisha Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) limekuwa likishirikiana na idara ya mahakama kutoa adhabu kwa wanaokiuka sheria na mikakati kuzuia Covid-19.

Aidha, baadhi ya wakazi Nairobi waliopatikana na hatia wamejipata kufanya shughuli za usafi wa mazingira jijini, kipindi cha muda wa wiki moja.

Serikali inaendelea kuhimiza wananchi kutii kanuni zilizopendekezwa na Wizara ya Afya kusaidia kuzuia msambao wa corona.

Zinajumuisha kuvalia maski – barakoa katika maeneo ya umma, kutakasa mikono kwa sabuni au jeli, kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake na kuepuka kukongamana maeneo yenye umati wa watu.

Machi 26, 2021 kwenye hotuba yake kwa taifa, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza zuio la kuingia na kutoka Kaunti za Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado na Nakuru, akizitaja kama hatari na zilizoshuhudia kiwango cha juu cha ongezeko la maambukizi.

Huku mwezi huu wa Machi ukikamilika, taifa limeandikisha idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya corona.

You can share this post!

Kampuni za dawa zaonya wananchi dhidi ya chanjo feki ya...

ODM yasema Raila amepona corona