Habari Mseto

Kamati nyingine ya upatanisho yabuniwa kujaribu kutanzua mzozo kuhusu ugavi wa fedha kwa kaunti

August 16th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA mara ya pili Spika wa Bunge la Kitaifa Jusitin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka wamebuni kamati nyingine ya upatanishi katika jitihada za kutanzua mzozo kuhusu ugavi wa fedha kwa kaunti.

Kamati hiyo yenye wanachama 18 ilibuniwa Alhamisi, siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuyataka mabunge hayo mawili kusuluhisha mvutano huo unaohusu kiasi cha fedha zinazofaa kutengewa serikali 47 za kaunti katika mwaka huu wa kifedha wa 2019/2020.

Bw Lusaka ameteua maseneta tisa ambao wataungana na wabunge tisa walioteuliwa na Bw Muturi ili kujaribu kujenga muafaka kuhusu suala hilo ambalo limesababisha changamoto za kifedha zinazoshuhudiwa katika serikali zote za magatuzi.

Mnamo Jumatano, Rais Kenyatta akiongea mjini Nakuru alizitaka kaunti kukubali mgao wa Sh316.5 milioni ambazo zilipendekezwa na Bunge la Kitaifa katika mswada wa ugavi wa mapato (DoRB) uliopitishwa kabla ya wabunge kwenda likizo.

“Ninaomba Bunge la Kitaifa na Seneti kukomesha mzozo huu ili kuokoa wananchi wanaoteseka katika ngazi za mashinani kwa kukosa huduma,” Rais akasema alipohutubu katika Ikulu ya Nakuru alipotumbuizwa na shule zilizoshinda katika Mashindano ya Muziki yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Kabarak.

Kubaini ugavi

Mswada wa ugavi wa mapato ni muhimu kwa sababu hubaini ugavi wa fedha baina ya serikali za kaunti na ilye ya kitaifa.

Mswada huo umekosa kupitishwa mara mbili baada ya maseneta kusisitiza kuwa kaunti zigawiwe Sh335 bilioni kufadhili huduma na miradi ya maendeleo katika kaunti hizo katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 ulioanza Julai mosi mwaka huu.

Lakini bunge la kitaifa nalo linashikilia kuwa kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni pekee, wabunge wakisema kuwa hatua hiyo inatokana na sababu kwamba Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) haikutimiza kiwango lengwa cha kodi mwaka 2018.

Bw Lusaka alitaja maseneta wafuatao kuwakilisha seneti katika kamati hiyo ya upatanisho; Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Fedha Mohamed Mahamud (Seneta wa Mandera), Charles Kibiru (Kirinyaga), Margaret Kamar (Uasin Gishu), Mithika Linturi (Meru), Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Ladema Ole Kina (Narok) Okongo Omogeni (Nyamira) na Rose Nyamunga (Seneta maalumu).

Watashrikiana na wabunge Aden Duale (Kiongozi wa Wengi), John Mbadi (Kiongozi wa wachache), Kimani Ichungwa (Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti), Junet Mohamed (Kiranja wa Wachache), Cecily Mbarire (Mbunge Maalum), Amos Kimunya (Kipipiri), Makali Mulu (Kitui ya Kati), David Sankok (Mbunge Maalum) na Mishi Mboko (Likoni).

Kipengee cha 113 cha Katiba kinatoa fursa kubuniwe kamati ya upatanisho endapo mabunge yote mawili yatakosa kukubaliana kuhusu mswada kuhusu ugavi wa mapato kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

Mnamo Juni 2019 kamati ya upatanisho iliyobuniwa ilikosa kupata muafaka kuhusu suala hilo.

Wanachama wa Seneti walilegeza msimamo na kukubali mgao wa Sh327 bilioni kwa kaunti huku wenzao wa bunge la kitaifa wakishikilia Sh316.5 bilioni.

Mvutano huo ulisababisha Waziri wa Fedha aliyesimamishwa kazi Henry Rotich kusoma bajeti ya kitaifa mnamo Juni 13, kabla ya kupitishwa kwa mswada huo.

Lakini katika bajeti hiyo Bw Rotich alizitengea serikali 47 za kaunti Sh310 bilioni pekee.

Hii ina maana kuwa endapo maseneta na wabunge watakubaliana kuhusu mgao wa Sh316.5 bilioni au Sh335 bilioni, kaimu Waziri wa Fedha Ukur Yattani atalazimika kuifanyia marekebisho bajeti ya mwaka huu kwa kupunguza mgao wa fedha zilizotengewa baadhi ya idara na wizara za serikali kupata pesa za kuongezea mgao wa kaunti.