Makala

Kamati ya Seneti iliyochunguza ufujaji wa fedha za afya ilivyojitetea

October 3rd, 2020 4 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Bungoma Moses Wetang’ula amekana taarifa kwamba Kamati maalum ya Seneti iliyochunguza sakata ya mpango wa ukodishaji wa vifaa vya kisasa vya matibabu kwa serikali za kaunti (MES) ilifyonza zaidi ya Sh30 milioni pesa za umma.

Kwenye mohojiano na Taifa Leo Ijumaa, Oktoba 2, 2020, kwa njia ya simu, Bw Wetang’ula alitaja taarifa kama za uwongo na zinazolenga kuwachochea wananchi dhidi ya maseneta “waliojitolea kwa mhanga kuchunguza hitilafu zilizokumbu mpango huo uliogharimu Sh63 bilioni.

“Vyombo vya habari vinapasa kukoma kuandika habari za kupotosha kuhusu kazi ya kamati hiyo ya Seneti. Tulifanya kazi nzuri na kuandaa ripoti ambapo tulipendekeza Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iwachungeza maafisa wote wa serikali waliohusika katika mpango huo. Sio ukweli kwamba kazi hiyo iligharimu zaidi ya Sh30 milioni,” akasema Seneta huyo alikuwa Naibu Mwenyekiti wa kamati ya wanachama tisa iliyoongozwa na Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo (pichani).

“Magazeti yakomeshe mtindo huu mbaya wa kuandika taarifa zisizo za ukweli na zinazolenga kuwaharibia sifa maseneta na kudunisha kazi wanayofanya kukinga wizi wa pesa za umma

Lakini tulipomtaka Bw Wetang’ula kufichua kiasi halisi cha fedha ambazo kamati hiyo ilitumia katika uchunguzi wake uliodumu mwaka mmoja, alituelekeza kwa Karani wa Seneti Jeremiah Nyengenye.

“Maelezo kamili kuhusu suala hilo yanaweza tu kupatikana katika afisi ya karani. Lakini ningependa kukuhakikishia kuwa kiasi cha fedha tulizotumia hazipiti Sh10 milioni,” akaeleza.

Lakini tulipojaribu kumfikia Bw Nyengenye, hakujibu simu zetu wala ujumbe mfupi tuliomtumia tukitaka maelezo kuhusu suala hilo.

Mnamo Alhamisi gazeti la The Star liliripoti kuwa zaidi ya Sh30 milioni, pesa za umma “zilipotea” katika uchunguzi wa mpango huo tata wa MES.

Lakini mnamo Jumanne maseneta walitupilia mbali ripoti hiyo yenye kurasa 395 baada ya kuijadili katika vikao viwili.

Japo Kamati hiyo ilitaja mpango huo kama “Biashara ya Uhalifu” (Criminal enterprise) ulioanzishwa kwa lengo la kufaidi maafisa fulani wa serikali, haikutaja majina ya maafisa hao.

Kulingana na ripoti hiyo maafisa hao walishirikiana na kampuni mbalimbali za kigeni na za humu nchini kuwasilisha bidhaa hizo kwa serikali za kaunti kwa bei ya juu kuliko iwapo kaunti hizo zingejinunulia vifaa hivyo.

Chini ya mpango huo ulioasisiwa na Serikali ya Kitaifa mnamo 2014, vifaa vya kisasa vya kutibu magonjwa sugu kama vile saratani vilisambazwa katika hospitali mbili za kiwango cha level 4 katika kila kaunti. Magavana wa kaunti 46 walitia saini mkataba wa maelewano kuhusu mpango huo isipokuwa kaunti ya Bomet, wakati huo ikiongozwa na kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto, kama gavana.

Kati ya miaka ya 2014 na 2015, mpango wa MES ulipokuwa ukitekelezwa, Waziri wa Afya alikuwa James Macharia (sasa Waziri wa Uchukuzi), Katibu wa Wizara akiwa Bi Khadijah Kassachon huku Mkurugenzi wa Matibabu akiwa Dkt Nicholas Muraguri (sasa Katiba katika Wizara ya Ardhi).

Katika ripoti yake kamati hiyo pia ilibaini kuwa sheria ya ununuzi wa bidhaa na huduma ilikiukwa katika mpango huo kwani baada ya kampuni zilizopewa zabuni kusambaza vifaa hivyo vya kimatibabu havikuwa vimehitimu kisheria..

Lakini wakichangia mjadala kuhusu ripoti hiyo, maseneta waliwasuta Bi Dullo na wenzake kwa kukosa kutaja majina halisi ya maafisa wa serikali wanaopasa kulaumiwa na kuwajibikia makossa yaliyokumba mpango huo wa MES.

“Bila kutaja majina ya maafisa waliotekeleza makosa na kuchangia wananchi kutofaidika kwa mpango huo, kamati hii imefanya kazi chapwa. Hii ni sawa na barua ya mapenzi,” akasema kiranja wa wachache katika seneti Mutula Kilonzo Junior.

Kwa upande wake, Seneta wa Nandi Samson Cherargei alisema ripoti hiyo inafanana na barua ya malalamishi kwani haina mapendekezo thabiti “ambayo yanaweza kusaidia kuadhibiwa kwa washukiwa.”

Naye Seneta wa Narok Ladema Ole Kina aliwalaumu wanachama wa kamati hiyo kwa kutotaja majina wa washukiwa katika sakata hiyo akisema hali hiyo “imetoa taswira mbaya kwamba huenda wanachama wa kamati huu walishawishiwa kwa njia moja ama nyingine.

Hatimaye maseneta walikataa kuidhinisha ripoti hiyo, hali ambayo iliwavunja moyo maseneta wengine waliokuwa wanachama wa kamati hiyo.

“Tunapoandaa ripoti yenye maelezo ya kina kama hii lakini maseneta wanaitupilia mbali, tunahisi kuwa tulipoteza wakati bila sababu yoyote. Tunaiachia hapo ikiwa hatua hiyo inaakisi matakwa ya Wakenya,” akasema Seneta wa Nyandarua Mwangi Githiomi.

Kamati hiyo ilifanya zaidi ya vikao 100 ambapo iliwahoji maafisa wa serikali na wakurugenzi wa kampuni ambazo zilipewa zabuni ya kusambaza vifaa hivyo vya matibabu. Isitoshe, uchunguzi huo uliwapeleka Bi Dullo na wenzake hadi Uholanzi ambako walikaa kwa siku tatu.

Kando na Wetang’ula, Githiomi na Bi Dullo (mwenyekiti), wanachama wengine wa kamati hiyo ambayo iliundwa mnamo Septemba 9, 2019 walikuwa; Christophe Lang’at (Seneta wa Bomet), Enock Wambua (Kitui), Stewart Madzayo (Kilifi) na maseneta maalum Millicent Omanga na Mary Seneta.

Kulingana na taarifa ya Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC) kuhusu marupurupu ya kuhudhuria vikao yanayolipwa wabunge na maseneta, mwenyekiti wa kamati hupokea Sh10,000 kwa kila kikao, naibu wake hupokea Sh8,000 na mwanachama wa kawaida hulipwa Sh5,000.

Ikizingatiwa kuwa kamati hiyo ilifanya zaidi ya vikao 100, ina maana kuwa mwenyekiti pekee alitia kibindoni Sh1 milioni kama marupurupu ya vikao huku naibu wake akipata Sh800,000.

Na kila mmoja wa wanachama kawaida alilipwa jumla ya Sh500,000.

Kwa ujumla wanachama wa kamati hiyo walitumia Sh5.3 milioni kama marupurupu ya kuhudhuria vikao pekee.

Wakati wa ziara yao Uholanzi, makao makuu ya kampuni ya M/s Philips Medical Systems ambayo ilisambaza vifaa vya kutumiwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) ya thamani ya Sh3.6 bilioni, kila mwanachama alilipwa Sh79,868 kila siku kwa siku tatu, kama marupurupu, maarufu kama “per diem”.

Kiasi hicho cha fedha ni kando la nauli ya ndege kutoka Nairobi hadi jijini Amsterdam na gharama ya chakula pamoja na malazi ambayo ililipwa na Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Kando na hayo mlipa ushuru alilipia nauli, malazi na chakula ya maseneta hao walipozuru kaunti za Meru, Trans Nzoia, Mombasa, Pokot Magharibi na Nairobi wakati wa uchunguzi huo kuthibitisha ikiwa kaunti hizo zilipokea vifaa hivyo vya MES ilivyodaiwa.

Wafanyakazi wa bunge kama vile makarani, walinzi, wasaidizi wa kibinafsi na walinzi wa wanaoandama na maseneta hao pia walilipwa kutokana na pesa za umma.

Awali, kamati hiyo ilitarajiwa kukamilisha uchunguzi wake kwa siku 45 pekee, hadi Novemba 12, 2019 lakini ikaomba muda zaidi, hadi Desemba 26, 2019. Kisha mnamo Januari 2, 2020 kamati hiyo ikaombo muda wa siku 45 zaidi ili iweze kukamilisha uchunguzi wake mnamo Machi, 2020.

Tena iliomba iongezewe muda wa siku 60 zaidi hadi Julai 14 na siku 21 za kuandika ripoti. Mamilioni ya fedha zilitumika nyakati hizo zote ambazo kamati ilikuwa ikiomba iongezewe muda zaidi kwa wanachama walikuwa wakisafiri humu nchini na mataifa ya nje wakiwahoji mashahidi.