Michezo

Kamati yaundwa kupokeza mamlaka Ingwe

May 28th, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Muungano wa wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi ujao wa klabu ya AFC Leopards, kwa ushirikiano na washikadau, Jumatatu usiku waliunda Kamati ya Muda ya Kupokeza Mamlaka (ATT) kwa viongozi watakaochaguliwa mwezi ujao wa Juni.

Kamati hiyo chini ya Vincent Shimoli itahakikisha kwamba katiba ya klabu hiyo inaambatana na Sheria Mpya za spoti nchini kama ilivyoagizwa na afisi ya Wizara ya Michezo mnamo 2018, lakini ikapuuzwa na Kamati Kuu ya klabu hiyo ya ligi kuu ya Kenya (KPL) inayodhaminiwa na SportPesa.

Katiba hiyo walisema itawasilishwa kwa wanachama wakati wa Mkutano Mkuu wa Klabu ili iidhinishwe rasmi ili ianze kutumika.

Kamati hiyo ya ATT itakayokuwa mamlakani kwa kipindi cha mwezi mmoja inatarajiwa kuidhinishwa rasmi Jumapili wakati wanachama wa klabu hiyo watakusanyika katika uwanja wa Railway Club, Nairobi kupanga mipango mikakati ya kuandaa mkutano mkuu wa klabu.

Siku hiyo, Jumapili, kadhalika kamati hiyo inatarajiwa kuteua Bodi ya kusimamia uchaguzi na kuwapa wanachama muda zaidi wa kujiandikisha kama wapigaji kura.

Mapendekezo hayo yalipitishwa wakati wanachama walikutana jijini Nairobi na watakaowania viti kwenye uchaguzi huo.

Kadhali, kikao hicho kiliwaitisha viongozi walio mamlakani kuondoka usukani kesho Jumatano mara tu baada ya ya mechi ya mwisho dhidi ya Western Stima na kumuachia uadhifa Afisa Mkuu wa Klabu jukumu la kulinda mali ya klabu.

Vile vile kikao hicho kiliwaamuru maafisa wa sasa wasijaribu kuwania viti wakati wa uchaguzi huo baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo na uongozi duni..

Mkutano huo pia ulikataa Kamati iliyoundwa na maafisa wa klabu Kuusimamia Uchaguzi ujao (EMG) huku ukidai kwamba iliundwa kwa upendeleo baada ya kugunduliwa kwamba waliopewa mamlaka hayo ni marafiki wa karibu wa viongozi wa klabu hiyo wanaonuia kuhifadhi viti vyao.