Makala

KAMAU: Afrika isiendelee kulaumu Wazungu kwa shida zake

August 28th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

UTUMWA ni suala nzito ambalo mara nyingi huibua hisia kali miongoni mwa wale waliushuhudia ama wanaoufahamu kwa undani.

Nazungumzia kizazi cha watu waliozaliwa kabla ya 1945, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilipokamilika.

Bila shaka, si watu wengi waliozaliwa enzi hizo wamebaki. Wengi wao wameaga dunia.

Hata hivyo, wachache waliosalia, hasa nchini Amerika na mataifa mengi barani Afrika, bado wana kumbukumbu hai kuhusu madhila ambayo Waafrika walifanyiwa na Waingereza, Waarabu, Wafaransa, Wahispaniola na Wareno walipotekwa nyara na kuuzwa kama watumwa.

Kwa mujibu wa historia, Wazungu walikuwa wakivamia jamii za Kiafrika na kuwateka nyara wanaume na kuwasafirisha hadi katika nchi zao, ambapo waliwauza kama mifugo.

Wakati mwingine, wavamizi hao waliripotiwa kuchoma vijiji hivyo na kuwabaka ama hata kuwaua wanawake na watoto.

Kimsingi, huu ni udhalimu ambao kamwe hauwezi kusahaulika, hasa miongoni mwa kizazi ambacho kilishuhudia madhila hayo moja kwa moja.

Hata hivyo, inashtua kwamba mpaka sasa, Waafrika wengi bado wanawalaumu Wazungu kwa masaibu yanayozikumba nchi zao.

Wengi bado wanahusisha “utumwa na uvamizi wa Wazungu” wakidai ni chanzo kikuu cha baadhi ya masaibu yanayoziandama nchi zao kama utawala mbaya, ufisadi, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, kudorora kwa uchumi kati ya maovu mengine.

Ni suala alilorejelea mwanamuziki Aliaume Damala, maarufu kama ‘Akon’ mzaliwa wa Senegal anayeishi Amerika wiki iliyopita. Alisema kuwa, Waamerika Weusi wanapaswa kujaribu kusahau athari za utumwa ili kuanza ukurasa wa ufanisi mpya kihistoria, kisiasa na kijamii.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha habari Amerika, Akon alisema kuwa, kinyume na Waamerika Weusi, Waafrika wengi tayari wamesahau mateso waliyopitia chini ya tawala za kikoloni.

Alisema Weusi wanapaswa kuwaiga Waafrika, kwa kusahau madhila hayo, ambapo mengi yalifanyika mwanzoni mwa ya karne ya 20.

Licha ya kauli hiyo, mwanamuziki huyo amekosolewa vikali na baadhi ya makundi ya Waafrika na Waamerika Weusi, wakimtaja kuwa “msaliti na msahaulifu kuhusu historia.”

Kwa kweli, huu ni mdahalo mzito. Ni suala linaloibua hisia kali, ikizingatiwa kwamba, Amerika bado inaendelea kushuhudia visa na udhalimu unaohusiana na ubaguzi wa rangi, kama vile mauaji ya kukeketa maini ya mwanaume mweusi George Floyd mnamo Mei.

Hata hivyo, imefikia wakati makundi haya mawili yaanze kuwa na mtazamo mpya kuhusu mwelekeo wake kihistoria na kijamii.

Kwa kauli ya Akon, hayawezi daima kuendelea kuwalaumu Wazungu kwa madhila yaliyotokea karibu karne moja iliyopita kuwa chanzo cha changamoto zinazowaathiri.

Badala yake, imefikia wakati yasuluhishe tofauti hizo na wale walioyatesa ili kuwa na mwanzo mpya.

Kwa mfano, nchi nyingi za Afrika zimejiongoza zenyewe tangu 1960 wakati mataifa mengi yalipata uhuru bila uwepo wa Wazungu. Amerika nayo imepiga hatua kubwa kiasi cha kuwa na rais mwenye asili ya Kiafrika, Barack Obama.

Je, ni vipi tena tutaendelea kuwalaumu Wazungu kwa changamoto zetu daima dawamu? Tufungue ukurasa mpya wa maridhiano.

[email protected]