Makala

KAMAU: Inasikitisha kuona waliopigania demokrasia wakiivuruga

May 29th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MIKAKATI inayoendelezwa na baadhi ya vyama vya kisiasa nchini “kuwaadhibu” wanachama wanaodaiwa kukiuka “kanuni na masharti” imedhihirisha kuwa vyama hivyo ni taasisi ambazo zinadhibitiwa na viongozi wake.

Hili limedhihirishwa wazi na Chama cha Jubilee (JP), ambacho kimewachukulia hatua kali viongozi hao, kwa kuwatoa katika kamati muhimu kwenye Seneti.

Baada ya ‘kusafisha’ uwakilishi wake kwenye Seneti, inadaiwa kwamba chama kitaelekeza mjeledi wake kwenye Bunge la Kitaifa.

Na kama kuiga Jubilee, vyama tanzu vya muungano wa Nasa pia vimetangaza kuanza mchakato kama huo.

Hata hivyo, kilicho wazi ni kwamba “usafishaji” huo ni mbinu fiche ya kuwaadhibu wabunge na maseneta ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto.

Mchakato huu wote umedhihirisha wazi kuwa licha ya Kenya kupiga hatua kubwa katika uwepo wa vyama vingi ya kisiasa nchini, msingi wa uwepo wa vyama huru vyenye misingi na taasisi thabiti ni ndoto ambayo bado haijatimizwa.

Ni mkasa kuu kuwa hali hii inatokea karibu miaka thelathini baada ya mamia ya watu kuhatarisha maisha yao wakipigania ‘kombozi wa Pili’.

Mkasa mwingine pia ni kuwa mwelekeo huo unadhihirika miaka kumi tu baada ya Kenya kupata katiba mpya mnamo 2010.

La kushangaza ni kuwa, chama cha ODM, anachoongoza Bw Raila Odinga, ni miongoni mwa vile ambavyo vimechukua mwelekeo huo.

Hiki ni kinaya kikuu kwani kando na kuongoza harakati za kushinikiza urejeo wa vyama vingi vya kisiasa, Bw Odinga vile vile alikuwa mfungwa wa kisiasa chini ya utawala wa Daniel Moi.

Ikizingatiwa kuwa hali hii inafanyika wakati Bw Odinga anapaswa kuwa kielelezo mwafaka cha uendeshaji wa demokrasia nchini, hili linaachilia kuwa ndoto walizokuwa nazo wanaharakati hao bado hazijafikiwa.

Kama mmoja wa watu walioshiriki na hata kudhulumiwa akitetea kurejeshwa kwa mazingira huru ya kisiasa nchini, Bw Odinga anapaswa kutoa mwelekeo wa kufufua upya ndoto za wanaharakati hao.

Isipokuwa ni viongozi kama Bi Martha Karua na Bw Koigi Wamwere ambao wamedumisha misimamo na falsafa zao za kisiasa, wengi kati ya wanaharakati hao wamebaki kimya ama mateka wa mfumo wa kisiasa za ubinafsi.

Vyama kamwe havifai kuwa kama vyombo vya ulipizaji kisasi. Vinapaswa kuwa kiunganishi cha watu na ishara ya umoja wao.

[email protected]