KAMAU: Kuna ishara ghasia za 2007/08 zitatokea tena

KAMAU: Kuna ishara ghasia za 2007/08 zitatokea tena

Na WANDERI KAMAU

UWAJIBIKAJI wa serikali husika hukitwa katika namna ambapo taasisi huru huendesha majukumu yake.

Ni vibaya ikiwa taasisi zilizobuniwa kuwahudumia wananchi zitaonekana kutumiwa na mrengo fulani wa kisiasa “kuwaadhibu” na kuwahangaisha washindani wao.

Katika historia ya Kenya, moja ya tatizo kuu ambalo limekuwa likiiandama nchi hii ni wananchi kukosa imani na utendakazi wa taasisi za umma zilizopo.

Kwa mfano, moja ya sababu zilizosababisha ghasia za baada ya uchaguzi tata wa urais wa 2007 ilikuwa ni viongozi kukosa imani na taasisi kuu kama Idara ya Mahakama.

Wakati huo, kiongozi wa ODM, Raila Odinga, alisema hangeweza kwenda mahakamani kwani alihisi hangepata haki kwenye malalamishi yake kuwa uchaguzi huo uligubikwa na wizi wa kura.

Hilo ndilo lililowafanya wafuasi wake kukasirika vibaya kwani walihisi hata ikiwa Bw Odinga angeenda mahakamani, uamuzi ambao ungetolewa ungempendelea Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Hilo ndilo lililochangia taharuki ya kisiasa kuongezeka katika sehemu mbalimbali nchini, ambapo baadaye iligeuka kuwa moja ya mapigano mabaya zaidi ya kikabila na kisiasa kuwahi kushuhudiwa nchini.

Bw Odinga na washirika wake katika kundi la ‘Pentagon’ walihisi kuwa taasisi muhimu kama Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK), Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), Jeshi la Kenya (KDF), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kati ya zingine zilikuwa zikimuunga mkono Bw Kibaki.

Tatizo lilo hilo ndilo lililosababisha ghasia za kisiasa na kikabila zilizotokea katika miaka ya 1992, 1997, 2013 na 2017.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 1992, vigogo wakuu wa kisiasa walimlaumu marehemu Daniel Moi kwa kutumia ushawishi wake kuzishinikiza taasisi muhimu kama ECK kutoa matokeo ya kura yaliyoonyesha aliibuka mshindi kwenye uchaguzi huo.

Mtindo huo bila shaka ulijenga mazingira ambayo wanachi walipoteza imani kabisa na taasisi muhimu za serikali.

Vivyo hivyo, kuna hatari ya Wakenya kupoteza imani tena na taasisi hizo, hata ikiwa zinaendeshwa kwa msingi na mwongozo wa Katiba ya 2010.

Sababu kuu ni kuwa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta unaonekana kutumia taasisi kama DCI, Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Halmashauri ya Kukusanya Ushuru (KRA) kuwahangaisha wanasiasa ambao wanaipinga serikali yake ama wamegeuka kuwa wakosoaji wake.

Ingawa siegemei upande wowote wa kisiasa, ni wazi sasa vita dhidi ya ufisadi nchini vinaendeshwa kwa ubaguzi na kwa maonevu ya wazi dhidi ya wakosoaji wa Rais Kenyatta.

Kwa mfano, maswali yanaibuka kuhusu sababu ya mbunge Rigathi Gachagua (Mathira) kufunguliwa mashtaka ya ufisadi mara tu baada ya chama cha Jubilee kushindwa vibaya katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kiambaa na UDA.

Mbona hakukamatwa kabla ya uchaguzi huo?

Mwelekeo huu ni hatari, hasa wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Je, itakuwa vipi ikiwa viongozi watakaoshindwa kwenye uchaguzi huo watakataa kukubali matokeo ya uchaguzi wa urais?

Wito wetu ni kwa Rais Kenyatta kutoirejesha Kenya kwenye giza la 2007/2008.

akamau@ke.nationmedia.com

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa wajiepushe na mjadala...

AKILIMALI: Kilimo cha pilipili chabadilisha maisha ya...