Makala

KAMAU: Ufisadi nchini umegeuka zimwi litakalomeza wote

September 26th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

UFISADI ni mbaya.

Ufisadi huua. Ufisadi ni kama saratani ya kimaadili inayomkeketa mwanadamu wa sasa.

Mkasa mkuu wa maradhi ya saratani ni kuwa hayatibiki. Ayapatapo mtu, mara nyingi huanza kujitayarisha kuondoka duniani kwa nafsi yake mwenyewe.

Kenya ni kioo halisi wa mgonjwa wa saratani kimaadili. Saratani yake ni ufisadi.

Ni ugonjwa ambao umekataa kutibika. Ufisadi umejaa serikalini, kwenye dini na hata sekta za kibinafsi.

Ufisadi umegeuka sehemu ya mtindo wa maisha nchini. Kwa namna nyingine, ufisadi ni sehemu ya ‘tamaduni’ kuu za Mradi Kenya.

Upeo wa ufisadi, ubinafsi na ukosefu wa thamani ya ubinadamu ulidhihirika Jumatatu, baada ya wanafunzi wanane wa Shule ya Msingi ya Precious Talent jijini Nairobi kufariki baada ya kuangukiwa na madarasa yao.

Baada ya mkasa huo, ilidhihirika kuwa vyuma vilivyotumika kwenye ujenzi wa madarasa hayo havikufaa, baadhi ya wahandisi wakisema kuwa vinatumika kujengea vyumba vya kuku!

Lawama zilifuata. Viongozi wa serikali waliofika walitoa rambirambi kwa familia zilizoathiriwa na kukashifu vikali utaratibu uliofuata katika ujenzi wa shule hiyo.

Kwa upande wake, mmiliki alijitetea vikali, akisema kiini cha kubomoka kwa madarasa hayo si udhaifu wa vyuma vilivyotumika, mbali ujenzi wa mtaro wa kubebea maji taka unaochimbwa karibu na shule hiyo.

Mkasa huo uligeuka kuwa jukwaa la lawama na majibizano badala ya kuzua mdahalo wa mikakati ya kukagua mfumo wa ujenzi katika shule zote nchini.

Kinaya ni kwamba, hii si mara moja ambapo jumba lililojengwa vibaya limebomoka na kusababisha maafa jijini Nairobi na kwingineko nchini.

Umekuwa ni kama mtindo, Kenya kuchukulia kwa uzito jambo pale mkasa unapotokea.

Hilo linaposahaulika, maisha huendelea kama kawaida. Mkasa mwingine hubisha hodi. Ahadi zinatolewa. Maonyo yanatoka kila sehemu. Kila aina ya tahadhari hutolewa, lakini zote hugeuka kuwa kelele na abrakadabra butu ambazo huwa hazina maana yoyote kwa waathiriwa.

Uchungu mkuu katika mkanganyiko huu wa ukosefu wa sera bora za kukabiliana na mikasa ni kuwa, mifumo iliyopo inahimiliwa na ufisadi.

Uidhinishaji

Kwa mfano, inadaiwa maafisa wa kusimamia na kuidhinisha ujenzi wa majengo katika idara nyingi serikalini huwa hawafuatilii ubora wa majengo yanayojengwa, ikiwa mjenzi atawahonga kwa kiwango fulani cha pesa.

Hilo hufuatia uwepo wa majengo dhoofu ambayo hubomoka kwa urahisi na kuwaua watu baada ya muda fulani.

Uozo huo pia umetaasisika katika mfumo wa matibabu nchini, ambapo madaktari wamekuwa wakiwatibu watu magonjwa tofauti na yale wanayougua. Katika nyakati zingine, wamekuwa wakiwashauri watu hao kufanyiwa upasuaji, hata ikiwa hawafai!

Kimsingi, tumegeuka jamii ya wanyamapori. Upori umeufanya ubinadamu kuadimika kwa kila namna. Maisha ya mwanadamu hayathaminiwi tena, bora tu anayehusika atajirike.

Tu Jamhuri ya Unyama na Ushetani. Jamii isiyovijali vizazi vyake vijavyo. Ni kama mama awalaye wanawe. Ni nani atatukomboa?

 

[email protected]