KAMAU: UhuRuto wasiturejeshe enzi ya Moi kuhusu urithi

Na WANDERI KAMAU

HUENDA kitabu ‘The Kenyatta Succession’ (Harakati za Urithi wa Mzee Jomo Kenyatta) ndicho kinachochora taswira kamili ambayo huwepo wakati siasa za urithi zinapokaribia nchini.

Katika kitabu hicho ambacho kiliandikwa na marehemu Philip Ochieng na James Karimi, waandishi wanaelezea kwa kina jinsi kundi la wanasiasa kutoka Mlima Kenya lilivyofanya kila juhudi kumzuia marehemu Daniel Moi kuchukua uongozi baada ya kifo cha Mzee Kenyatta mnamo 1978.

Kundi hilo lilijiita ‘Change the Constitution Movement’ na lilikuwa likiishinikiza serikali kuibadilisha Katiba ili kuondoa uwezekano wa Moi kumrithi Kenyatta.

Ingawa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wakati huo, Bw Charles Njonjo, alifanikiwa kutumia mamlaka yake kuwazima wanasiasa hao, utawala wa Moi ndio ulikuwa mwanzo wa masaibu, mahangaiko na madhila yaliyomwandama yeyote aliyejitokeza kumpinga Moi na utawala wa chama cha Kanu.

Kuanzia 1978, Kenya iligeuka kutoka taifa la kidemokrasia hadi nchi iliyofanana na falme iliyoongozwa na mfalme ambaye asingekosolewa na yeyote.

Kwa miaka 24 aliyoitawala Kenya, marehemu Moi alifanya kila awezalo kumkabili na ‘kumnyamazisha’ yeyote aliyeonekana kutoridhishwa na utawala wake.

Kilichofuata ni vita vya kikabila, jaribio la mapinduzi ya kijeshi, mateso dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na mauaji ya wanasiasa waasi.

Udhalimu

Udhalimu wa utawala wa Moi ulifikia kiwango ambapo wananchi na jamii ya kimataifa walianza kumshinikiza kurejesha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa nchini.

Kabla ya kuchukua hatua hiyo mnamo 1992, Moi alikuwa amesukumwa hadi mwisho na mataifa yenye ushawishi mkubwa wa kisiasa duniani kama Amerika na Uingereza.

Nchi hizi zilitishia kusimamisha misaada ya kifedha kwa Kenya ikiwa Moi asingeruhusu uwepo wa vyama vingi vya kisiasa.

Cha kusikitisha ni kuwa, tunaonekana kurejea katika enzi hizo kwa mara nyingine.

Sarakasi zinazoendelea kumwandama Naibu Rais William Ruto zinaashiria kuwa huenda akajipata pale pale Moi alipokuwa mnamo 1978.

Kadri siasa za urithi wa Rais Uhuru Kenyatta zinavyoendelea kushika kasi, ndivyo taswira iliyomwandama Moi inavyoendelea kudhihirika.

Hilo limedhihirishwa na matukio mawili makuu—kisa ambapo Ruto alizuiwa kusafiri kuenda Uganda na kufurushwa kwa mshirika wake Mturuki kutoka Kenya, Harun Aydin.

Bila shaka, ingawa huenda matukio haya yote yanatokana na habari za kijasusi na tishio dhidi ya uthabiti wa kisiasa nchini, lazima asasi husika zihakikishe sarakasi hizi hazigeuki kuwa chemchemi ya machafuko ya kisiasa nchini.

Kama washirika na marafiki wa kisiasa wa muda mrefu, Rais Kenyatta anamfahamu kiundani Dkt Ruto. Vivyo hivyo, Dkt Ruto anamfahamu kwa kina Rais Kenyatta—pamoja na udhaifu wake.

Wawili hawa wamekuwa washirika wa karibu wa kisiasa tangu mwaka 2002, wakati Rais Kenyatta aliwania urais kwa tiketi ya Kanu ijapokuwa alishindwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Wito wetu ni kwa wawili hawa kutoelekeza tofauti na ghadhabu zao kwa wananchi.

Vile vile, tunawarai wasihatarishe uthabiti wa kisiasa uliopo nchini, kwa kuturejesha katika enzi za giza kama ilivyokuwa wakati wa urithi wa Mzee Kenyatta.

Kenya ni kubwa kuliko kiongozi yeyote na itadumu milele hata watakapoondoka.

akamau@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii