Makala

KAMAU: Vijana wazinduke sasa kuzikomboa jamii zao

November 24th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KATIKA historia, vijana wameibukia kuwa waendeshaji wakuu wa harakati za ukombozi katika nchi zao.

Sababu halisi ni kuwa wao huwa na ufahamu kamili kuhusu mwelekeo unaoifaa jamii na wanajamii waliopo wakati huo.

Hivyo, wakati jamii inajipata katika mkwamo wa maovu yanayohusiana na utawala mbaya, tegemeo kuu huwa hatua watakazochukua vijana.

Wanapoungana ili kuyakemea maovu hayo na kuwashinikiza viongozi walio mamlakani kung’atuka ama kuwajibika, hilo huwa afueni kubwa kwa jamii.

Hata hivyo, mkasa mkuu huwa wanapoamua kunyamazia dhuluma na madhila wanayopitia katika jamii.

Mfano halisi wa vijana walioleta mageuzi ya kiutawala katika jamii zao ni Alexander the Great na Thomas Sankara.

Alexander, aliyeitawala nchi ya Macedonia, anakumbukwa kwa kuongoza harakati za kijeshi kubuni mojawapo ya falme kubwa zaidi duniani.

Ingawa alitumia wanajeshi kwenye harakati zake, inaelezwa aliwasaidia watu maskini waliotelekezwa na watawala wa falme alizoziangusha.

Alipanua ufalme wake kutoka Ugiriki hadi Persia na Misri.

Mtawala huyo alifariki akiwa na umri wa miaka 32 pekee.

Barani Afrika, Sankara atakumbukwa daima kwa harakati zake katika kuwatetea na kuwakomboa watu maskini nchini Burkina Faso katika miaka ya themanini.

Alipoteuliwa kuhudumu kama Waziri Mkuu wa taifa hilo mnamo 1983, mzozo mkali uliibuka katika serikali alimokuwa akihudumu.

Serikali hiyo ilikuwa ikilaumiwa pakubwa na raia kwa tuhuma za ufisadi na kutojali maslahi yao.

Aliwekwa kizuizini kwa kuonekana kama “aliyewachochea” raia kuipinga.

Mwaka uo huo, baadhi ya raia na wanaharakati waliochoshwa na utawala huo waliongoza mapinduzi kwa niaba yake.

Kwa kipindi alichoitawala nchi hiyo kati ya 1983 na 1987, alileta mageuzi makubwa; baadhi yakiwa sera za kijamaa kuwainua watu maskini, kubadilisha jina la taifa hilo kutoka Upper Volta hadi Burkina Faso kuonyesha kujisimamia kwake dhidi ya kasumba za kikoloni kati ya mafanikio mengine.

Aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa na umri wa miaka 37 pekee mnamo 1987.

Bila shaka, mifano hiyo miwili inaashiria vijana wana jukumu kubwa katika kuikomboa jamii dhidi ya maovu yanayoikumba.

Natoa urejeleo huo kutokana na misukosuko ya kisiasa inayoendelea kushuhudiwa katika mataifa mengi Afrika, hasa kabla na baada ya chaguzi kuu.

Kiundani, mizozo hiyo inawaathiri vijana na usemi wao kwa namna moja ama nyingine.

Baadhi ya nchi hizo ni Nigeria, Tanzania, Uganda na Ethiopia.

Nchini Nigeria, maelfu ya vijana wanaandamana kulalamikia ukatili wa Kikosi Maalum cha Kukabiliana na Uhalifu (SARS), wanachokitaja kama njama ya serikali kuwahangaisha.

Nchini Tanzania, serikali ya Rais John Magufuli inalaumiwa pakubwa kuweka vikwazo katika utumizi wa mitandao wa kijamii, huku waathiriwa wengi wakiwa vijana.

Nchini Uganda, mwanamuziki Bobi Wine anawaongoza vijana nchini humo kwenye harakati za kumkabili Rais Yoweri Museveni.

Je, sauti na juhudi za vijana wa Kenya zi wapi?

Ni wakati wawaige wenzao kwingineko Afrika ili kuzikomboa jamii zao dhidi ya maovu na utawala mbaya.

[email protected]