KAMAU: Viongozi sasa waelekeze macho kwa umoja wa taifa

Na WANDERI KAMAU

UMOJA wa nchi ni msingi ambao kila mmoja anapaswa kuzingatia.

Bila umoja, nchi huwa kama ombwe tu—jamii isiyo na mwelekeo wowote hata kidogo.

Ukosefu wa umoja, mshikamano na uthabiti wa kisiasa ndio umevuruga ustawi uliokuwepo awali katika nchi kama Somalia, Yugoslavia, DRC Kongo, Sudan, Sudan Kusini kati ya nyingine.

Nusura Kenya ijipate hapo baada ya ghasia zilizotokea kutokana na uchaguzi tata wa 2007.

Lengo kuu la urejeleo huu linatokana na majibizano makali ambayo yamekuwa yakishuhudiwa miongoni mwa wanasiasa kuhusu Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI).

Kwa miaka mitatu iliyopita, viongozi wamegawanyika katika mirengo tofauti ya kisiasa —kwa msingi wa wale waliounga ama kupinga mchakato huo.

Kila mrengo uliukosoa mwenzake kwa “kuendeleza ubinafsi” kulingana na msimamo uliochukua.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ndio waliowaongoza viongozi walioupigia debe mchakato huo, huku Naibu Rais William Ruto akiwaongoza wale walioupinga.

Ikizingatiwa uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, Ijumaa iliyopita kufutilia mbali mchakato huo ni kama umeusimamisha, kuna haja viongozi kuungana tena na kutathmini upya mwelekeo wa nchi.

Viongozi wanapaswa kufahamu kuwa hakukuwa na mshindi yeyote kutokana na uamuzi huo, kwani mageuzi hayo ya kikatiba yalihusu mwelekeo na mustakabali wa nchi.

Ni mageuzi ambayo pia yangeviathiri pakubwa vizazi vijavyo, wakati viongozi waliopo hawatakuwepo tena mamlakani.

Ingawa kuna fasiri kwamba nyota ya kisiasa ya Dkt Ruto imeimarika pakubwa kutokana na uamuzi huo, imani yangu ni kuwa mshindi mkuu ni Katiba ya Kenya.

Maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa mtawalia yanaonyesha kuwa si rahisi kwa kiongozi yoyote kuigeuza Katiba atakavyo bila kufuata taratibu zote zilizowekwa.

Kwa utathmini wa kina, moja ya sababu ambazo zimekuwa zikichangia mapigano katika baadhi ya nchi ulimwenguni ni mtindo wa viongozi kubadilisha katiba ili kuendelea kukwamilia mamlakani.

Katika nchi ya Somalia, nusura mapigano kuzuka upya mapema mwaka huu wa 2021, baada ya Rais Mohamed Farmaajo kuahirisha uchaguzi mkuu katika hali tatanishi.

Uchaguzi huo ulikuwa umepangiwa kufanyika mwezi Februari.

Nchini Ethiopia, hali inaendelea kudorora kutokana na mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea katika eneo la Tigray.

Je, tunataka kuchukua mikondo hiyo?

Ukweli ni kuwa, si vigumu Kenya kujipata hapo, ikiwa viongozi hawatatilia maanani umuhimu wa kuheshimu maamuzi yanayotolewa na taasisi huru kama mahakama.

akamau@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii