KAMAU: Vyombo vya habari vyafaa viwajibike 2022 ikikaribia

KAMAU: Vyombo vya habari vyafaa viwajibike 2022 ikikaribia

Na WANDERI KAMAU

MOJA ya sababu kuu ambazo zilisababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mnamo 1994 ilikuwa ni mchango uliotolewa na vyombo vya habari.

Kwenye ripoti mbalimbali ambazo ziliandikwa baada ya mauaji hayo na mashirika kama Umoja wa Mataifa (UN), Amnesty International (AI), Human Rights Watch (HRW) kati ya mengine, redio zilizopeperusha matangazo yake kwa lugha asili ndizo zililaumiwa pakubwa kwa kueneza chuki.

Chuki na uhasama huo ndio ulisababisha jamii za Wahutu na Watutsi kugeukiana na kuuana bila kujali wao ni ndugu wanaoishi katika nchi moja.

Lawama zaidi zilielekezwa kwa kituo cha redio cha RTL (Free Radio and Television of the Thousand Hills) ambacho kiliaminika kutumika na maafisa wakuu wa serikali ya Rwanda kueneza chuki dhidi ya Watutsi.

Kituo hicho kiliaminika kusaidiwa na Radio Rwanda kueneza propaganda dhidi ya jamii hiyo.

Vituo hivyo vinaaminika kutumika kueneza jumbe kwa wapiganaji wa Kihutu, ambazo ziliwasaidia kujua mahali ambapo watu waliowalenga walikuwa wamejificha.

Katika hali hiyo, ni wazi kuwa vyombo vya habari huwa na athari kubwa kwa jamii, na jumbe zake hutegemewa sana na hadhira yake.

Vyombo hivyo pia viliaminika kutumika pakubwa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia (1914-1918) na Vita vya Pili vya Dunia (1939-1945).

Wasomi wa historia, siasa, utawala na mahusiano ya kimataifa wamekuwa wakisema mbinu iyo hiyo ndiyo imekuwa ikitumika katika maeneo mbalimbali duniani ambayo yameshuhudia vita baada ya 1945.

Cha kushangaza ni kuwa, Kenya ni miongoni mwa maeneo hayo.

Mbinu hiyo inaelezwa kutumika kwenye vita vilivyotokea nchini baada ya uchaguzi tata wa 2007, ambapo baadhi ya vyombo vya habari vililaumiwa pakubwa kutumika na wanasiasa kueneza chuki dhidi ya jamii ambazo hazikuwaunga mkono kisiasa.

Huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukiendelea kukaribia, kumeibuka hofu kuwa baadhi ya vyombo vya habari nchini vimeanza kuonyesha wazi mirengo ya kisiasa vinavyounga mkono.

Kama hatua ya “kulipiza kisasi”, baadhi ya wanasiasa hata wameanza kususia vipindi na mijadala ya kisiasa wanayoalikwa katika vyombo hivyo kutokana na tuhuma hizo.

Bila shaka, huu si mwelekeo wa kuridhisha hata kidogo. Si hali ya kutia moyo, ikizingatiwa tumeanza kushuhudia visa vya mauaji ambavyo vinahusishwa na uchaguzi huo.

Kwa mfano, mashambulio yanayoshuhudiwa katika Kaunti ya Laikipia kati ya wakulima na jamii za kuhamahama yametajwa kuchochewa na baadhi ya wanasiasa ili “kuwaondoa watu wanaochukuliwa kuwa wageni katika eneo hilo.”

Ingawa serikali imetangaza kafyu kati ya saa 12 jioni hadi saa 12 alfajiri, mwelekeo huo unapaswa kutufungua macho kuhusu janga linalotuandama ikiwa tahadhari za mapema hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo.

Taasisi muhimu kama Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CAK) zinapaswa kuzinduka na kudhibiti utendakazi wa vyombo vya habari.

Ripoti ya Jaji Philip Waki kuhusu ghasia za 2007/2008 ilizilaumu redio hizo kwa kueneza chuki baina ya mirengo iliyowaunga mkono Rais Mstaafu Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Ni wakati vyombo vya habari vifahamu vinaushikilia mustakabali wa taifa hili.

akamau@ke.nationmedia.com

You can share this post!

Hawana jipya hao, Mutua awasuta viongozi wa OKA

Wanasoka wa Chelsea na Bayern Munich wabeba Ujerumani dhidi...