Habari MsetoSiasa

Kambi achunguzwe na DCI, EACC – Wabunge

September 30th, 2019 1 min read

Na DAVID MWERE

BAADHI ya wabunge wanataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kuanzisha upelelezi utakaobainisha jinsi aliyekuwa Mbunge wa Kaloleni, Bw Kazungu Kambi alivyopata vyeti vya digrii kutoka vyuo viwili vikuu nchini.

Hii ni baada ya wabunge Teddy Mwambire (Ganze), Omar Mwingi (Changamwe) na Owen Baya (Kilifi Kaskazini) kukataa wiki iliyopita uteuzi wake katika Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kwa kutilia shaka vyeti vyake.

Watatu hao ni wanachama wa kamati ya bunge kuhusu ardhi, ambayo ilimhoji Bw Kambi.

Kwenye wasifu wake aliowasilisha bungeni, Bw Kambi alisema anaendelea kusomea uzamifu wa somo la fedha katika Chuo Kikuu cha Maseno.

Alidai pia kuwa alisomea uzamili wa usimamizi wa biashara (MBA) na digrii ya somo la maendeleo katika Chuo Kikuu cha Baraton.

Kilichofanya hayo yatiliwe shaka ni jinsi alivyokosa kueleza alisomea mambo hayo miaka ipi.

Jana, Bw Mwambire ambaye ni mpwa wake, alisema Bw Kambi hakuwasilisha vyeti vyake halisi na hivyo basi haijulikani jinsi alivyofuzu.

“Hatuwezi kuruhusu vyuo vikuu vya nchi hii vigeuzwe kuwa sehemu za kutakasa watu wasiofuzu. Ndiyo maana tunatoa wito kwa asasi za upelelezi serikalini ziiingilie kati, na watakaopatikana na kosa washtakiwe,” akasema.

Watu wote wanaoteuliwa kwa nyadhifa tofauti ambao hufika mbele ya bunge kupigwa msasa huhitajika kuwasilisha vyeti vyao halisi na kutaja miaka ambayo walisomea katika vyuo wanavyotaja.

Bw Kambi pia hakuwasilisha cheti chake cha Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) ijapokuwa alidai kupata alama ya D.