Habari Mseto

Kambi ya muda yabuniwa kuokoa waathiriwa wa mafuriko

April 30th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kitaifa kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Lamu imebuni kambi ya muda katika eneo la Nagele, tarafa ya Witu ili kuwaokoa waathiriwa wa mafuriko eneo hilo.

Zaidi ya wakazi 3000 waliachwa bila makao baada ya nyumba zao kusombwa na maji kwenye vijiji vya Chalaluma, Dide Waride, Moa na Matabore, Kaunti ya Lamu.

Mafuriko hayo yanasababishwa na kuvunjika kwa kingo za mito inayokaribiana na vijiji hivyo, ikiwemo ule mkubwa wa Tana na Nyongoro.

Akizungumza na Taifa Leo mapema Jumatatu, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono, alisema wameafikia hatua ya kubuni kambi hiyo kijijini Nagele kwani eneo hilo liko katika sehemu ya mwinuko na salama hasa wakati huu ambapo mafuriko yamekuwa yakihangaisha wakazi.

Bw Rono alisema kambi hiyo pia imebuniwa ili iwe rahisi kwa waathiriwa wa mafuriko hayo kusaidiwa na serikali na wahisani.

Aliwataka wakazi kwenye vijiji vyote vinavyoshuhudia mafuriko kuhama mara moja na kufika kambini badala ya kusubiri hadi maafa yawafikie.

“Tumeafikia kuanzisha kambi ili kuwapokea waathiriwa wa mafuriko. Ni vigumu kwetu kufika kwenye vijiji husika kuwasilisha misaada kutokana na ugumu wa usafiri msimu huu wa mafuriko.

Ningetaka watu kuhama sehemu hizo hatari na waje Nagele hadi pale hali shwari itakaporejea. Serikali tayari imetuma magunia ya mchele Nagele ili kukimu wale ambao tayari wamefika kambini humo. Tunajiandaa kuwasilisha misaada zaidi huko,” akasema Bw Rono.

Naye Afisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu, Tawi la Lamu, Kauthar Alwy, aliwalalamikia baadhi ya waathiriwa wa mafuriko hayo kwa kudinda kuhama kwenye vijiji vyao.

“Tangu wiki jana, tumekuwa tukiwaonya wakazi dhidi ya kuendelea kuishi kwenye sehemu zao ambazo zinashuhudia mafuriko. Licha ya kwamba nyumba zao zimesombwa na maji, idadi kubwa ya waathiriwa hawataki kuhama sehemu hizo.

Kama shirika inakuwa vigumu kuwafikia waathiriwa na kuwasaidia. Ikiwa watakubali kuhama na kuja Nagele, itakuwa rahisi kwao kusaidiwa na hali kudhibitiwa,” akasema Bi Kauthar.

Afisa huyo alisema wako tayari kutoa mahema wakati wowote punde idadi ya wakimbizi wa mafuriko itakapotathminiwa eneo hilo la Nagele.

Kwingineko, Kaunti ya Lamu imetuma maafisa wake kwenye vijiji vyote vinavyokumbwa na mafuriko ili kukusanya ripoti itakayosaidia kupeleka misaada kwa waathiriwa.

Afisa wa Kaunti katika Wadi ya Witu, Bw Hussein Roba, alisema tayari amezuru Moa, Chalaluma na Dide Waride ili kutathmini hali na kukusanya ripoti.

“Hali si shwari kwa sasa. Mafuriko yameathiri wakazi wengi. Tunakusanya ripoti ili kuona ni jinsi gani serikali ya kaunti pia itasaidia wahanga wa mafuriko eneo hili,” akasema Bw Roba.